Kuna mtu anaamini Mo Salah habaki
Muktasari:
- Tim Sherwood anaamini kwa uhakika kuwa nyota huyo wa Misri ataamua kuhitimisha safari yake Anfield mwaka huu. Sherwood alisema hana shaka hata kidogo kwamba Salah ataondoka, akidai ana uhakika wa asilimia 100 kuwa mshambuliaji huyo atachagua kuanza ukurasa mpya.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA, Mohamed Salah anaendelea kuhusishwa na mpango wa kuondoka Liverpool wakati wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi, licha ya kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Anfield.
Tim Sherwood anaamini kwa uhakika kuwa nyota huyo wa Misri ataamua kuhitimisha safari yake Anfield mwaka huu. Sherwood alisema hana shaka hata kidogo kwamba Salah ataondoka, akidai ana uhakika wa asilimia 100 kuwa mshambuliaji huyo atachagua kuanza ukurasa mpya.
Tetesi kuhusu mustakabali wa Salah zimekuwa nyingi tangu alipomkosoa kocha Arne Slot mapema msimu huu. Hali ilitulia baada ya mahojiano makali Desemba mwaka jana ambapo Salah alimshutumu Slot kwa kutaka kumwondoa kwenye timu.
Baada ya kurejea kutoka katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Salah amerudi katika kikosi cha kwanza cha kocha huyo Mdachi.
Ingawa hajafikia viwango vya kushangaza alivyokuwa navyo msimu uliopita kwa upande wa mabao, Salah alifunga na kutoa asisti katika ushindi wa Kombe la FA dhidi ya Brighton mwishoni mwa wiki, ishara ya kurejea kwenye kiwango chake.
Hata hivyo, Sherwood, ambaye ni kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur anaamini kurejea kwake kikosini hakubadilishi chochote kuhusu mustakabali wake, aliposema: “Weka wazi, nafikiri yeye ni miongoni mwa wachezaji bora wa kigeni tuliowaona katika Ligi Kuu England. Hakuna shaka kwamba kiwango chake kimeshuka msimu huu. Kumekuwa na masuala kati yake na kocha, bila kujali ni nini hasa. Nadhani kwa asilimia 100 ataondoka kiangazi hiki na naamini sasa anamalizia safari yake kwa heshima.”
Kwa upande mwingine, nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk alisema anatamani Salah abaki Anfield hadi mwisho wa mkataba wake licha ya tetesi zinazoendelea, aliposema: “Hali ilivyo ndivyo ilivyo. Kipaumbele chetu kikubwa ni kuifanya msimu huu uwe wa mafanikio, halafu tutaona mambo yatakavyokwisha. Mimi nataka Mo abaki kwa sababu ni rafiki yangu mzuri na tumepitia mengi pamoja kwa miaka mingi.”