Kumbe Mo Salah ameomba radhi
Muktasari:
- Kikosi hicho cha kocha Arne Slot kilikuwa kwenye kiwango cha hovyo na kujikuta ikikumbana na vipigo vizito kutoka kwa Nottingham Forest na PSV Eindhoven. Vipigo hivyo vilimfanya kocha huyo wa Kidachi kuamua kubadilisha kikosi chake na hivyo kuamua kumwaanzishia benchini mshindi wa Kiatu cha Dhahabu wa msimu uliopita, Mo Salah.
LIVERPOOL, ENGLAND: KIUNGO wa Liverpool, Curtis Jones amethibitisha Mohamed Salah amewaomba radhi wachezaji wenzake wa Liverpool kutokana na matamko yake aliyotoa mwanzoni mwa mwezi huu.
Kikosi hicho cha kocha Arne Slot kilikuwa kwenye kiwango cha hovyo na kujikuta ikikumbana na vipigo vizito kutoka kwa Nottingham Forest na PSV Eindhoven. Vipigo hivyo vilimfanya kocha huyo wa Kidachi kuamua kubadilisha kikosi chake na hivyo kuamua kumwaanzishia benchini mshindi wa Kiatu cha Dhahabu wa msimu uliopita, Mo Salah.
Mo Salah alianzia benchi kwenye mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu England dhidi ya West Ham, Sunderland na Leeds United. Aliingia kwenye mechi moja tu kati ya hizo, lakini mahojiano aliyofanya huko Elland Road, Desemba 6, yaliibua mjadala mzito baada ya kumshushia lawama Slot na kudai hana uhusiano naye mzuri na alifichua uwezekano wa kuondoka kwenye timu wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa.
Mo Salah alisema ni kama anashushwa vile kwenye basi na kwamba hahitajiki tena jambo lililomfanya kocha Slot kumweka kando kabisa kwenye kikosi chake kilichosafiri kwenda kumenyana na Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya mazungumzo ya Mo Salah na kocha Slot, alitumika kwenye mechi Brighton alipotokea benchi na kuasisti bao la Hugo Ekitike kwenye mechi ya ushindi wa mabao 2-0.
Salah kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Misri kitakachoshiriki mashindano ya Afcon 2025 huko Morocco na mikikimikiki hiyo itafika tamati Januari 18. Liverpool yenyewe kwa Jumamosi ilikuwa na mechi ngumu dhidi ya Tottenham na kiungo Jones alisema Mo Salah aliwaomba radhi wachezaji wenzake kabla ya kuondoka, hivyo hawana shida naye.
"Mo ni mwanamume na anaweza kusema mambo yake," alisema Jones. "Alituomba radhi na kusema kama kuna yeyote alimkwaza, basi asamehewe. Ni mwanamume wa aina hiyo."