Kufukuzwa kazi kumempa Mourinho Sh337 bilioni
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 62 aliondoka Fenerbahce ya Uturuki jana ikiwa ni siku mbili tu baada ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Benfica.
ISTANBUL, UTURUKI: KOCHA Mreno, Jose Mourinho yuko karibu kufikisha Pauni 100 (takriban Sh337 bilioni) kama malipo ya fidia ya kufukuzwa kazi tangu aanze maisha ya ukocha.
Kocha huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 62 aliondoka Fenerbahce ya Uturuki jana ikiwa ni siku mbili tu baada ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Benfica.
Mourinho aliwasili Istanbul 2024 ikiwa ni miezi sita baada ya kufutwa kazi na AS Roma, na kipindi chote alichokaa ameshindwa kushinda taji lolote, lakini anatarajiwa kulipwa fidia nono kwa kuvunjiwa mkataba.
Kwa mujibu wa gazeti la michezo la Uturuki, Fanatik, Mourinho atapokea kitita cha fidia cha Pauni 12 milioni.
Katika maisha yake ya ukocha yenye mafanikio makubwa kocha huyo amejipatia kiasi kikubwa kupitia fidia za kufutwa kazi na timu mbalimbali ambazo kwa mjumuisho pamoja na hiyo ya Fenerbahce imefikia Pauni 100 milioni.
Akiwa Chelsea alipata Pauni 26.3 milioni katika vipindi vyake viwili alivyofukuzwa na fidia kubwa zaidi aliyowahi kupata ilikuwa ile aliyolipwa na Manchester United katika msimu wake wa tatu, ambapo alipokea Pauni 19.6 milioni.
Alipokuwa kocha wa Real Madrid alikunja Pauni 17 milioni kama fidia ya kuvunjiwa mkataba na mabingwa hao wa Hispania wakati huo, ilhali pale Tottenham Hotspur alipokea Pauni 15 milioni, huku Roma ikimlipa fidia ndogo zaidi ya Pauni 3 milioni.
Mourinho amefukuzwa na Fenerbahce baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Benfica katika mchezo wa mkondo wa pili kufuatia suluhu kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wiki iliyopita iliyopigwa Istanbul.
Taarifa zinadai Mourinho huenda akarejea England, lakini mara hii itakuwa ni katika timu ambazo hazishiriki Ligi ya Mabingwa.
Oktoba mwaka jana alikaririwa akisema: "Jambo bora zaidi naloweza kufanya nitakapoondoka Fenerbahce nitaenda klabu isiyoshiriki mashindano ya UEFA. Kwa hiyo, kama kuna klabu yoyote England hata zile za mwisho kwenye msimamo zikihitaji kocha baada ya miaka miwili niko tayari."