Kone ‘mguu wake umening’inia’ Vancouver
Muktasari:
- Mashabiki waliojazana katika Uwanja wa BC Place walibaki na mshangao mkubwa dakika ya 55 ya mchezo huo wa Kundi B baada ya Kone kulazimika kutolewa nje kwa machela kufuatia jeraha linalodhaniwa kuwa la kuvunjika mguu.
FURAHA ya Canada kupata ushindi wake wa kwanza kabisa katika Kombe la Dunia iligubikwa na simanzi kubwa baada ya kiungo nyota Ismael Kone kupata jeraha baya la kutisha wakati wa ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Qatar.
Mashabiki waliojazana katika Uwanja wa BC Place walibaki na mshangao mkubwa dakika ya 55 ya mchezo huo wa Kundi B baada ya Kone kulazimika kutolewa nje kwa machela kufuatia jeraha linalodhaniwa kuwa la kuvunjika mguu.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 alianguka chini akishika mguu wake wa kushoto kwa maumivu makali baada ya kuchezewa faulo mbaya kutoka nyuma na mchezaji wa Qatar, Assim Madibo, katika dakika ya 51.
Baada ya mchezo, kocha wa Canada, Jesse Marsch, alisema tukio hilo lilimuumiza sana na hata kudai alisikia mfupa wa mchezaji wake ukivunjika.
"Moyo unaumia kwa ajili yake. Kila mmoja amesikitika kutokana na kilichotokea," alisema Marsch huku akiongeza kuwa angeelekea hospitali moja kwa moja kumuangalia mchezaji huyo.
Mara baada ya jeraha hilo kutokea, wachezaji wa Canada waliinuka kwa hasira huku benchi la ufundi likilipuka kwa malumbano makali. Beki Richie Laryea alionekana akizuiwa na mchezaji wa Qatar alipokuwa akimkabili Madibo kwa hasira.
Wakati huohuo, madaktari waliingia haraka uwanjani kutoa huduma huku wachezaji wa Canada wakimzunguka Kone kwa hofu na majonzi. Rafiki yake wa karibu, Jonathan David, alionekana kushikwa na mshtuko mkubwa, huku beki kijana Luc de Fougerolles akishindwa kujizuia na kulia uwanjani kabla ya kufarijiwa na kipa Maxime Crepeau.
Baada ya kuwekwa kifaa maalumu cha kuimarisha mguu wake, Kone alitolewa nje kwa machela akiwa amevaa barakoa ya oksijeni. Hata hivyo, alionesha moyo wa kishujaa kwa kuwapungia mkono mashabiki waliokuwa wakiimba jina lake kwa sauti kubwa.
Hasira ziliongezeka zaidi baada ya mwamuzi kumwonesha Madibo kadi ya njano pekee katika tukio la kwanza. Mmoja wa wasaidizi wa Marsch alisikika akipaza sauti kwa maafisa wa mchezo akisema: "Mguu wake umening’inia!"
Baada ya kupitia teknolojia ya VAR, kadi hiyo ya njano ilibadilishwa na kuwa nyekundu. Madibo mwenyewe alionekana kuvunjika moyo kwa tukio hilo, akisimama huku ameshika kichwa chake kwa masikitiko makubwa kabla ya kuondoka uwanjani akiwa analia.
Kutolewa kwa Madibo kulifanya Qatar kubaki na wachezaji tisa baada ya Homam Ahmed naye kupewa kadi nyekundu kipindi cha kwanza.
Kabla ya tukio hilo, Canada ilikuwa tayari inaongoza kwa mabao 3-0 kupitia bao la Cyle Larin na mawili ya Jonathan David.
Dakika chache baada ya Kone kuondoka, Nathan Saliba aliyeingia kuchukua nafasi yake aliifungia Canada bao la nne kwa mpira wa adhabu. Baada ya kufunga, Saliba aliadhimisha kwa hisia kubwa kwa kumbukumbu ya Kone, akinyanyua jezi yenye maandishi “KONE 8” mbele ya mashabiki waliomshangilia kwa nguvu.
Marsch alisema licha ya maumivu ya kumpoteza Kone, timu yake ilijitahidi kubaki makini.
"Kila mmoja aliumia sana kuona kile kilichotokea, lakini tulijua Ismael angependa tumalize kazi. Tunawaza sana kuhusu yeye, lakini pia tunajivunia utu na moyo ambao timu hii imeuonyesha leo," alisema kocha huyo.
Canada iliendelea kutawala mchezo huo, ikiongeza bao la tano kupitia kujifunga kwa Mohamed Manai kabla ya Jonathan David kukamilisha' hat-trick' yake dakika za nyongeza.
Hata hivyo, licha ya ushindi huo mkubwa, habari mbaya ya jeraha la Kone ndiyo imebeba uzito mkubwa zaidi kwa Canada. Kiungo huyo alikuwa mmoja wa wachezaji bora wa timu hiyo na alionekana kuwa silaha muhimu katika kampeni yao ya kwanza ya Kombe la Dunia wakiwa wenyeji.