Kocha Senegal aiweka Bafana Bafana listi ya mabingwa
Muktasari:
- Thiaw amesema ni jambo la kushangaza sana kuona wachambuzi wengi wakishindwa kuitaja Afrika Kusini kama moja ya timu zinazoweza kutoa ushindani mkubwa barani Afrika.
KOCHA Mkuu wa Senegal, Pape Thiaw ameonyesha kushangazwa na namna watu wengi wanavyoitoa timu ya taifa ya Afrika Kusini maarufu Bafana Bafana katika orodha ya timu zinazotajwa kuwa na uwezo wa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Thiaw amesema ni jambo la kushangaza sana kuona wachambuzi wengi wakishindwa kuitaja Afrika Kusini kama moja ya timu zinazoweza kutoa ushindani mkubwa barani Afrika.
Wakati Thiaw akiyasema hayo, Kocha wa Bafana Bafana, Hugo Broos, amesema wao hawapo miongoni mwa timu anazoziona kuwa ni vigogo wa kutwaa taji hilo licha ya kuwa kwenye rekodi ya kucheza mechi 20 bila kupoteza katika mashindano rasmi na kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano ya mwisho.
Thiaw ambaye enzi za uchezaji wake alikuwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Senegal, ameisifu Bafana Bafana kwa ubora wa soka lao, akibainisha mshikamano mkubwa uliopo ndani ya kikosi hicho ni silaha muhimu.
Kocha huyo ameeleza, wachezaji wengi wa Afrika Kusini wanatoka kwenye klabu zilezile za ndani, jambo linalosaidia kuongeza maelewano, mshikamano na nidhamu ya kiufundi uwanjani.
Aidha, Thiaw amegusia kile alichokiita upendeleo unaojirudia mara kwa mara katika uchambuzi wa soka la Afrika na wachezaji wanaocheza barani Ulaya hupewa uzito mkubwa zaidi kuliko wale wanaocheza ndani ya Afrika, hata kama kiwango chao ni cha juu.
Akirejea historia ya hivi karibuni, kocha huyo alikumbusha kuwa Bafana Bafana ilimaliza nafasi ya tatu kwenye AFCON iliyopita, jambo linalothibitisha ubora na uzoefu wao katika mashindano makubwa.
Kwa mujibu wa Thiaw, mafanikio hayo pekee yanatosha kuipa Afrika Kusini heshima na kuitambua kama timu yenye uwezo wa kufika hatua za juu na hata kupigania ubingwa kwenye michuano ijayo.
BROOS AGOMA
Kwa upande wa Broos, alisema: “Ni hatari sana kujitangaza mwenyewe kuwa ni mshindani mkubwa wa taji. Hilo linafaa kufanywa na vyombo vya habari au mashabiki. Kitu pekee ninachoweza kusema ni kwamba AFCON hii itakuwa ngumu zaidi kuliko ile ya Ivory Coast.”
Alifafanua sababu akisema: “Najua kwa nini. Nadhani mataifa makubwa hayatarudia makosa waliyofanya hapo awali. Kama mnakumbuka, mataifa mengi makubwa hayakufuzu au yaliondolewa mapema. Naizungumzia Misri, Cameroon, Ghana, Morocco na mengineyo. Hilo halitatokea safari hii. Nadhani wamejifunza somo lao.”
Ingawa Broos hayuko tayari kuiweka Afrika Kusini katika orodha ya vigogo wa ubingwa, ana mtazamo wazi kuhusu timu anayoiona ina nafasi kubwa zaidi ya kutwaa taji.
“Hilo linamaanisha, kwa kawaida ingawa hakuna cha kawaida katika mashindano kama haya, timu zote kubwa zitafuzu baada ya hatua ya makundi. Hivyo, itakuwa ngumu sana kushinda AFCON hii.
“Ikiwa kuna timu moja ya kuitaja kuwa inaweza kuwa bingwa, basi ni Morocco, kwa sababu ni timu nzuri sana na inacheza nyumbani. Kwa wengine wote, itakuwa ni changamoto.”
Aliongeza tathmini inaweza kubadilika kadri mashindano yanavyoendelea.
“Tutaona baada ya hatua ya makundi ni timu zipi zitakuwa bado zipo, ndipo labda tutabadilisha mtazamo wetu. Lakini kwa sasa, hamtanisikia nikisema Afrika Kusini ni miongoni mwa inayoweza kutwaa ubingwa.”
Bafana Bafana imeanza mashindano ya AFCON 2025 kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Angola ambapo sasa ina pointi tatu katika Kundi B sawa na Misri ambayo nayo iliipa Zimbabwe kichapo kama hicho.
Timu hiyo ilitwaa taji lao pekee la AFCON mwaka 1996, ilipokuwa mwenyeji wa mashindano hayo.