Kocha Madrid afunguka ishu ya Valverde, Tchouameni
Muktasari:
- Valverde na Tchouameni wamepigwa faini ya Euro 500,000 kila mmoja, baada ya kupigana kwenye uwanja wa mazoezi wa Real Madrid siku ya Alhamisi, tukio lililosababisha Valverde kupelekwa hospitali kutokana na jeraha la kichwa alilopata.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa amesema hatawasema vibaya wachezaji wake hadharani kufuatia ugomvi mkubwa uliotokea mazoezini kati ya Federico Valverde na Aurelien Tchouameni, lakini amekiri yeye ndiye anayebeba lawama kwa msimu mbaya wa timu hiyo.
Valverde na Tchouameni wamepigwa faini ya Euro 500,000 kila mmoja, baada ya kupigana kwenye uwanja wa mazoezi wa Real Madrid siku ya Alhamisi, tukio lililosababisha Valverde kupelekwa hospitali kutokana na jeraha la kichwa alilopata.
Ripoti kutoka Hispania zimeeleza mvutano huo ulianza siku moja kabla, baada ya Valverde kukataa kumpa mkono Tchouameni wakati wa salamu za kawaida za kikosi.
Baadaye katika mazoezi, wawili hao waliendelea kurushiana maneno na kuchezeana faulo.
Inaelezwa wakati walipowekwa timu moja katika mazoezi ya ndani, Valverde alimkejeli Tchouameni kabla ya hali kubadilika na kuanza kupigana.
Katika vurugu hizo, Valverde aligonga meza na kupata jeraha lililosababisha damu kutoka pamoja na kupoteza fahamu kwa muda mfupi, jambo lililowatia hofu baadhi ya wachezaji wenzake akiwemo Tchouameni mwenyewe.
Katika kurasa zake za mitandao ya ijamii, Valverde alisisitiza hakuna aliyempiga mwenzake ngumi katika tukio hilo.
Akizungumza kabla ya mechi yao dhidi ya Barcelona, Arbeloa aliwatetea wachezaji hao wawili na kusifu namna klabu ilivyoshughulikia suala hilo kwa haraka.
Arbeloa amesema wachezaji hao wameonyesha kwa miaka mingi maana ya kuwa sehemu ya Real Madrid na hawastahili kushambuliwa hadharani kutokana na kosa hilo.
Pia alisisitiza madai ya wachezaji kutokuwa na nidhamu au kutomheshimu yeye kama kocha si ya kweli.
Kocha huyo ameongeza yeye ndiye anayewajibika kwa timu kushindwa kufikia matarajio ya mashabiki msimu huu na wanaotafuta mtu wa kulaumiwa wanapaswa kumtazama yeye kwanza.
Wakati huo huo, ripoti nyingine zimehusisha beki wa Real Madrid Antonio Rudiger na ugomvi mwingine na mchezaji mwenzake Alvaro Carreras na inadaiwa Rudiger alimzaba kibao Carreras.
Arbeloa amesema migogoro ya ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo imekuwa sehemu ya kawaida katika soka kwa miaka mingi, akitoa mfano wa tukio la mwaka 2007 alipokuwa akiichezea Liverpool na Craig Bellamy alidaiwa kumpiga mwenzake John Arne Riise kwa fimbo ya gofu baada ya kukataa kuimba karaoke.
Hata hivyo, Arbeloa ameonyesha kukerwa na uvujishaji wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, akisema wanaofichua siri za ndani wanaisaliti nembo ya Real Madrid.