Kocha Chelsea alalamikia kona za Arsenal
Muktasari:
- Chelsea iliruhusu mabao yote mawili dhidi ya Arsenal kutokana na mipira ya kona katika kipigo cha 2-1 kwenye Ligi Kuu England , Jumapili.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa wa Chelsea, Liam Rosenior, ametaka kufanyike mapitio ya namna mipira ya adhabu inavyosimamiwa, akidai kuwa kwa sasa inazipa timu fulani faida isiyo ya haki.
Chelsea iliruhusu mabao yote mawili dhidi ya Arsenal kutokana na mipira ya kona katika kipigo cha 2-1 kwenye Ligi Kuu England , Jumapili.
Hata hivyo, bao la Chelsea pia lilitokana na mpira wa kona, ambapo kona ya Reece James iligongwa na beki wa Arsenal, Piero Hincapié na mpira kuingia nyavuni. Mchezo huo umeonyesha jinsi mipira iliyokufa ilivyozidi kuwa silaha muhimu katika Ligi Kuu England.
Bao la pili la Arsenal lililofungwa na Jurrien Timber lilikuwa bao la 16 la timu hiyo kutoka kona msimu huu, rekodi inayolingana na ya juu zaidi. Imeripotiwa pia kuwa kocha wa mipira iliyokufa wa Arsenal, Nicolas Jover, ana kipengele cha bonasi kwenye mkataba wake kwa kila bao la mtindo huo linapofungwa na timu hiyo.
Hata hivyo, kushikana na kuvutana kunakotokea wakati wa kona kulisababisha baadhi ya wachambuzi kuuita mchezo wa Jumapili kuwa usio wa kuvutia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rosenior alisema: “Nadhani huo ndio uzuri wa soka. Unaweza kulicheza kwa njia nyingi tofauti. Kwangu, hakuna njia sahihi au isiyo sahihi ya kucheza soka.
"Nina uhakika tulipofunga kwa kona, mpira ulipoguswa kidogo tu na kuingia, mashabiki wetu hawakujali bao lilionekanaje. Na nina uhakika mashabiki wa Arsenal hawakujali mabao yao yalionekanaje".
"Mchezo ni kuhusu kushinda. Lakini, ninachoweza kusema kuhusu kona ni kwamba nadhani kunahitajika mapitio mwishoni mwa msimu kuhusu namna timu zinavyoathiri makipa, na namna zinavyoshikana katika mipira ya kujilinda. Kwa sababu naona hilo linazipa timu fulani faida isiyo ya haki.”