Kiungo Baleba bado anaitaka Man United
Muktasari:
- Man United imeshindwa kunasa saini ya kiungo huyo wa kati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuhusishwa sana na Baleba.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Brighton, Carlos Baleba ameripotiwa yupo tayari kujiunga na Manchester United licha ya uhamisho wake kukwama kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Man United imeshindwa kunasa saini ya kiungo huyo wa kati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuhusishwa sana na Baleba.
Brighton iliweka wazi Baleba hajawekwa sokoni, hivyo iliamua kuweka bei ya Pauni 115 milioni kwa timu itakayohitaji saini ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon.
Brighton ilihitaji ilipwe pesa kama ambayo ilivuna kwenye mauzo ya kiungo mkabaji Moises Caicedo aliponaswa na Chelsea.
Hata sasa wakati dirisha la usajili likiwa limefungwa bado Man United inapiga hesabu za kurudi tena kwa kiungo huyo, ambaye pia ameweka wazi milango ya kutua Old Trafford.
Baleba, 21, hakuwamo kwenye kikosi cha Cameroon kilichoshinda dhidi ya Eswatini, mechi ambayo iliwashuhusia Bryan Mbeumo na Andre Onana wakiitumikia timu hiyo ya taifa.
Mbeumo, ambaye alisajiliwa kwa ada ya Pauni 71 milioni na Man United katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, aliasisti wakati Cameroon iliposhinda 3-0.