Kisa semenyo, mmoja akamatwa
Muktasari:
- Mechi hiyo ya Ligi Kuu England ilisimamishwa kwa muda wa dakika 29 baada ya Semenyo, 25, kuripoti unyanyasaji huo kwa refa, Anthony Taylor, ambaye baadaye aliwaambia makocha wa timu zote mbili juu ya hilo.
LIVERPOOL, ENGLAND: POLISI katika Jiji la Liverpool, wamethibitisha mwanamume mmoja amekamatwa baada ya Antoine Semenyo kuripoti ubaguzi aliokutana nao wakati timu yake ikicheza dhidi ya Liverpool, kwenye dimba la Anfield, Ijumaa ya wiki iliyopita.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu England ilisimamishwa kwa muda wa dakika 29 baada ya Semenyo, 25, kuripoti unyanyasaji huo kwa refa, Anthony Taylor, ambaye baadaye aliwaambia makocha wa timu zote mbili juu ya hilo.
Baada ya mechi hiyo, ambayo Semenyo alifunga mabao mawili, mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana aliweka taarifa akishukuru mashabiki kwa msaada wao.
“Bila shaka, usiku wa jana Anfield utabaki ndani ya moyo wangu milele – siyo kwa maneno ya mtu mmoja, bali kwa jinsi familia yote ya soka ilivyoshikamana pamoja,” Semenyo aliandika.
“Kwa wachezaji wenzangu wa Bournemouth waliokuwa nami katika wakati huo, wachezaji na mashabiki wa Liverpool waliokuwa wakiungana namimi, maafisa wa Ligi Kuu walioshughulikia suala hili niseme asanteni. Soka lilionyesha upande wake bora wakati ulipohitajika zaidi...tunaendelea kusonga mbele, pamoja.”
Polisi wa Merseyside walithibitisha shabiki mmoja wa Liverpool aliondolewa Anfield kutokana na tukio hilo.
Jioni ya Jumamosi, polisi pia walitoa taarifa nyingine ikieleza inamshikilia mwanamume mwenye umri wa miaka 47 kutokana na tuhuma za ubaguzi.
“Tumemkamata mwanaume mmoja baada ya kupata ripoti za ubaguzi wa rangi aliofanyiwa mchezaji wa Bournemouth, Antoine Semenyo wakati wa mechi ya timu yake dhidi ya Liverpool katika Ligi Kuu England iliyofanyika Anfield Ijumaa ya Agosti 15,” ilieleza taarifa hiyo ya Polisi.