Kisa maji ya moto, Atletico Madrid yaishtaki Arsenal UEFA
Muktasari:
- Kikosi cha Diego Simeone kipo jijini London kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal itakayopigwa baadae leo Jumanne, Oktoba 21, 2025.
Atletico Madrid imekasirishwa na hali iliyoikuta katika uwanja wa Emirates na tayari imemewasilisha malalamiko rasmi kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) dhidi ya Arsenal, kwa kuwaacha wakitumia maji ya baridi kwenye mabafu.
Kikosi cha Diego Simeone kipo jijini London kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal itakayopigwa baadae leo Jumanne, Oktoba 21, 2025.
Kama ilivyo desturi, timu hiyo ya LaLiga ilifanya mazoezi kwenye uwanja wa Emirates jana jioni, kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mechi dhidi ya wenyeji wao, itakayounguruma Uwanja wa Emirates.
Hata hivyo, baada ya mazoezi yao, wachezaji wa Atletico walikumbwa na mshangao mkubwa walipokuta mabafu hayakuwa na maji ya moto.
Kwa mujibu wa gazeti la Marca kutoka Hispania, imeelezwa kuwa wachezaji na maofisa wa Atletico Madrid walikuwa na hasira sambamba na kushtushwa na tukio hilo, huku wakihoji inakuwaje Uwanja wa kisasa kama Emirates unaweza kukosa huduma ya msingi kama maji ya moto.
Maofisa wa Atletico walitoa taarifa kwa Arsenal jana saa 12:45 jioni, muda mfupi baada ya mazoezi kuanza, kwamba hakuna maji ya moto, huku mazoezi ya kikosi cha Simeone yalipangwa kuisha saa 1:30 usiku, lakini wachezaji walirudi vyumbani dakika 15 baadae na kugundua tatizo halikuwa limefanyiwa kazi.
SunSport inaelewa kuwa maji ya moto yalirejea saa 1:25 usiku, lakini tayari wachezaji wa Atletico walikuwa wameamua kuondoka uwanjani wakiwa bado wana jasho na kwenda kuoga hotelini.
Tayari Arsenal imeshaomba radhi kwa tukio hilo, ikisisitiza kuwa kadhia hiyo haikuwahi kutokea katika uwanja wao wa Emirates hapo awali.
La kufurahisha ni kwamba, kocha Simeone kwa miaka mingi anajulikana kwa kutumia mbinu za ujanja ujanja uwanjani, lakini mara hii amekuwa mhanga.
Ingawa baadhi ya wachezaji wa Atletico waliondoka Emirates wakiwa na hasira, wachafu na wenye baridi, inaonekana kuwa tatizo hilo lilikuwa la kiufundi na si njama yoyote.
Arsenal inakutana na Atletico ikiwa na rekodi ya kushinda mechi mbili za mwanzo za Ligi ya Mabingwa, huku Atletico ikipoteza mechi yao ya mwisho ilicheza England, ikifungwa 3-2 na Liverpool.
Licha ya Atletico kutoridhishwa na mapokezi waliyoyapata Emirates, kocha wa Arsenal Mikel Arteta amemsifu sana kocha wa Atletico kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi.
Arteta, mwenye umri wa miaka 43, amesema: “Bila shaka, (Simeone) ni mtu ninayemheshimu na kujifunza mengi kutoka kwake. Kitu kinachonivutia zaidi ni shauku yake ya kufanya kazi.
"Kwa muda ambao amekuwa kwenye mchezo huu, na ndani ya klabu hiyo hiyo, akiwa na baadhi ya wachezaji wale wale, bado ana uwezo wa kuwahamasisha kwa kiwango kikubwa.
"Tunaishi kwenye mazingira magumu sana, na kuendelea kuwashawishi wachezaji kwa kiwango kile kile ni jambo la kipekee.”