Kisa Gyokeres Man United yamgeukia huyu

Muktasari:
- Ekitike ambaye anaripotiwa kuuzwa kwa Pauni 80 milioni, saini yake pia inahitajika na Chelsea pamoja na Liverpool ambazo zinafanya mazungumzo na Frankfurt ili ikubali kupunguza bei.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United wameonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike, baada ya kufahamishwa Viktor Gyokeres anatamani zaidi kujiunga na Arsenal.
Ekitike ambaye anaripotiwa kuuzwa kwa Pauni 80 milioni, saini yake pia inahitajika na Chelsea pamoja na Liverpool ambazo zinafanya mazungumzo na Frankfurt ili ikubali kupunguza bei.
Fundi huyu wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alijiunga na Frankfurt kwa Pauni 14 milioni akitokea Paris Saint-Germain, msimu uliopita, alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 22.
Msimu uliopita alimaliza akiwa mfungaji kinara wa Frankfurt Bundesliga, akilingana na Omar Marmoush, ambaye alijiunga na Manchester City Januari mwaka huu.
Kocha mkuu wa Man United, Ruben Amorim, alikuwa akihitaji kuungana tena na Gyokeres baada ya timu yake kumaliza katika nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu na kupoteza fainali ya Europa League.
Lakini matumaini ya mashetani hao wekundu kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden yanaonekana kufifia, hivyo, nguvu zao wameelekeza kwa Ekitike licha ya bei yake kubwa.
Ekitike aliwahi kuulizwa ni timu gani aliyokuwa akiipenda alipokuwa mtoto akajibu kwa haraka ni Manchester United.
Inaeleweka Arsenal inaendelea na mazungumzo na Sporting kuhusu Gyokeres, ingawa Benjamin Sesko wa RB Leipzig anasalia kuwa chaguo lao la kwanza.
Iwapo watashindwa kufikia makubaliano na Leipzig, wanaweza kumrudia Gyokeres, ambaye alifunga mabao 54 katika mechi 52 kwa klabu yake msimu uliopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 pia anawaniwa na Juventus na timu kutoka Saudi Arabia.
Man United, ambao hawatashiriki michuano ya Ulaya msimu ujao wanaendelea kufanyia kazi dili la kumsajili mshambuliaji wa Brentford, Bryan Mbeumo kama sehemu ya maboresho ya safu yao ya ushambuliaji.
Hata hivyo, katika dili la Mbeumo wanakutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Tottenham na ofa yao ya Pauni 55 milioni waliyowasilisha mapema wiki iliyopita ilikataliwa.