Kinda Nigeria hajazikwa, mpenzi, rafiki mbaroni
Muktasari:
- Udoh aliyefariki muda mfupi tangu alipotua nchini humo, Mei 25, kwa likizo akitokea Czechoslovakia alikokuwa anaichezea Dynamo Ceske Budejovice inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, hajazikwa hadi sasa wakati mama yake akishinikiza uchunguzi wa kina ufanyike kujua nini kilichomuua.
ABUJA, NIGERIA: Kifo cha straika wa zamani wa Southampton na Nigeria, Victor Udoh kimeendelea kuzua maswali nchini humo ikiwa ni wiki moja tangu alipofariki dunia.
Udoh aliyefariki muda mfupi tangu alipotua nchini humo, Mei 25, kwa likizo akitokea Czechoslovakia alikokuwa anaichezea Dynamo Ceske Budejovice inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, hajazikwa hadi sasa wakati mama yake akishinikiza uchunguzi wa kina ufanyike kujua nini kilichomuua.
Mchezaji huyo aliyewahi pia kuichezea Royal Antwerp ya Ubelgiji alikuta akiwa amekufa nyumbani kwake muda mfupi alipotokea matembezini usiku ikiwa ni saa chache tangu alipowasili Abuja kutoka Czech.
Uchunguzi wa tukio hilo umechukua mkondo wa kisheria baada ya mama wa marehemu kufungua kesi dhidi ya mpenzi wa mwanaye huyo pamoja na rafiki wa karibu akitaka mamlaka za Nigeria kuwachunguza na kuchukulia hatua akiwatuhumu kuhusika na kifo chake.
Kufuatia kesi hiyo, mpenzi wa Udoh pamoja na mmoja wa marafiki zake wa karibu walikamatwa na kuwekwa mahabusu ambako wanashikiliwa wakati uchunguzi na upasuaji wa mwili wa marehemu kujua chanzo cha kifo ukisubiri amri ya mahakama.
Familia ya marehemu inaamini huenda kulikuwa na mchezo mchafu na inataka ukweli kamili kuhusu saa za mwisho za maisha ya kijana huyo ujulikane. Kwa sasa, maofisa wanaochunguza sakata hilo hawajaondoa uwezekano wowote, lakini nadharia ya sumu kupitia chakula au pombe inachunguzwa kwa umakini.
Inaelezwa kwamba matokeo ya uchunguzi wa maiti yanayotarajiwa kutolewa hivi karibuni yatasaidia kubaini chanzo halisi cha kifo hicho na kuthibitisha kama tuhuma za sumu zina msingi au la. Hadi sasa, hakuna sababu rasmi ya kifo iliyotangazwa na mamlaka husika.