Kane kupewa kibunda abaki zake Bayern
Muktasari:
- Nahodha huyo wa England kwa sasa ana mkataba na klabu hiyo ya Ujerumani unaoendelea hadi mwaka 2027.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA wa England, Harry Kane anatarajiwa kupata ongezeko kubwa la mshahara baada ya kuanza mazungumzo ya mkataba mpya katika klabu yake anayochezea kwa sasa huko Ujerumani, Bayern Munich.
Nahodha huyo wa England kwa sasa ana mkataba na klabu hiyo ya Ujerumani unaoendelea hadi mwaka 2027. Hata hivyo, Bayern inataka kumfunga kwa mkataba wa muda mrefu zaidi baada ya kufanya vizuri sana tangu alipojiunga mwaka 2023 kwa ada ya uhamisho ya Pauni 104 milioni akitokea Tottenham Hotspur.
Kane mwenye miaka 32 tayari amefunga mabao 130 katika mechi 133 alizocheza Bayern na kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa ligi ya Bundesliga msimu huu akiwa na mabao 30.
Kwa mujibu wa gazeti la Bild, Bayern iko tayari kuongeza mshahara wake wa Pauni 400,000 kwa wiki, ambao tayari unamfanya Kane kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika Bundesliga. Kane aliamua kutotumia kipengele cha kuvunja mkataba kilichokuwa kwenye mkataba wake, ambacho kilimalizika mwishoni mwa mwezi Januari.
Nyota huyo aliyechezea mechi 112 za kimataifa tayari ana utajiri unaokadiriwa kuwa zaidi ya Pauni 100 milioni. Nyaraka zinaonyesha kuwa kampuni yake ya haki za picha iitwayo HK28 Limited ilikuwa na akiba ya Pauni 11,428,513 benki mwishoni mwa mwaka 2024.
Katika mwaka huo pia, uwekezaji wake uliongezeka kutoka Pauni 2.8 milioni mwaka 2023 hadi Pauni 5.1 milioni. Kane pia ana ushirikiano wa kibiashara na kampuni ya Ujerumani 3Bears Foods GmbH, ambapo ameonekana kwenye tangazo la bidhaa yao ya uji.
Taarifa za mali zinaonyesha kuwa ana Pauni 2.2 milioni taslimu, huku uwekezaji wake katika majengo na mali zisizohamishika ukifikia Pauni 15 milioni mwaka 2024. Mkataba wake wa kwanza aliotia saini Bayern ulihakikisha mshambuliaji huyo analipwa angalau Pauni 86 milioni.