Kane amuweka chini Haaland Bundesliga
Muktasari:
- Staa huyo wa England ameandika rekodi nyingine ya kibabe kabisa huko Bayern Munich baada ya kufunga mabao kwenye mawili mechi yake ya 50 kwenye Bundesliga na hivyo kumfanya afikishe mabao 55 kwenye ligi hiyo tangu alipojiunga kutokea Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England.
MUNICH, UJERUMANI: KITU ambacho ni sahihi kumwelezea straika Harry Kane ni kumwita jina la ‘mtambo wa mabao’.
Staa huyo wa England ameandika rekodi nyingine ya kibabe kabisa huko Bayern Munich baada ya kufunga mabao kwenye mawili mechi yake ya 50 kwenye Bundesliga na hivyo kumfanya afikishe mabao 55 kwenye ligi hiyo tangu alipojiunga kutokea Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England.
Kane alifikisha mechi yake ya 50 ya Bundesliga kwenye mchezo wa ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Holstein Kiel uwanjani Allianz Arena.
Katika mechi hiyo, Bayern iliwachukua dakika 19 tu kufunga bao la kwanza kupitia kwa Jamal Musiala, lakini mwenye shoo yake Kane alitupia kwenye dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza kwa kichwa akiunganisha krosi tamu ya Kingsley Coman. Hilo lilikuwa bao la 54 kwake kwenye Bundesliga.
Jambo hilo lilimfanya Kane kwanza kuweka rekodi ya kwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika mechi zake 50 za kwanza kwenye Bundesliga.
Kuona haitoshi, ilimchukua sekunde 43 tu kwenye kipindi cha pili kufunga tena na kufikisha bao lake la 55 huku akiifanya Bayern kuongoza kwa mabao matatu. Hapo, Kane alijiweka pazuri na kumpiku straika Erling Haaland kwa kufunga mara nyingi kwenye mechi 50 za kwanza kwenye Bundesliga.
Haaland aliwahi kutamba kwenye Bundesliga kwa kipindi cha miaka miwili alipokuwa Borussia Dortmund kabla ya kunaswa na Manchester City mwaka 2022.
Hata hivyo, straika Haaland alifunga mabao 50 katika mechi 50 za kwanza kwenye Bundesliga.
Namba zinaonyesha kwamba, Kane amekuwa moto kwa mabao msimu huu, ambapo amefunga mara 19 katika mechi 18 za ligi.