Juve yawa shubiri kwa Luiz, Alisha
Muktasari:
- Wawili hao, wote wamekumbana na mwanzo mgumu wa maisha mjini Turin, na mmoja wao, hasa Douglas Luiz huenda akatemwa mapema tu. Luiz wakati akiwa Aston Villa chini ya Unai Emery alikuwa tegemeo katika kushambulia na ulinzi akihusika katika mabao 20 kwenye michuano yote 2023-24 na kuipa klabu mafanikio yaliyoshangaza wengi.
TURIN, ITALIA: UHAMISHO wa wanasoka wawili wapendanao, Douglas Luiz na Alisha Lehmann wa kutua Juventus umegeuka kuwa shubiri miezi michache tu tangu wasajiliwe kutoka Aston Villa.
Wawili hao, wote wamekumbana na mwanzo mgumu wa maisha mjini Turin, na mmoja wao, hasa Douglas Luiz huenda akatemwa mapema tu. Luiz wakati akiwa Aston Villa chini ya Unai Emery alikuwa tegemeo katika kushambulia na ulinzi akihusika katika mabao 20 kwenye michuano yote 2023-24 na kuipa klabu mafanikio yaliyoshangaza wengi.
Ili kukwepa kukatwa pointi kwa kukiuka sheria za mapato na matumizi, Villa ikalazimika kumuuza Douglas Luiz kwa Pauni 42 milioni kwenda Juve.
Na mpenziwe, Alisha aliyekuwa akichezea Villa ya wanawake akamfuata baada ya klabu hiyo ya Turin kumkubalia Luiz ombi la kumsajili mwanadada huyo. Juve ilivutika pia kwa ajili ya kujitangaza, kwani mrembo huyo mwenye shepu ya kuvutia ana wafuasi milioni 17 katika mitandao yake ya kijamii.
Lakini tangu atue Juve, Luiz amecheza mechi tisa tu, huku mbili tu akianzishwa.
Na mbaya zaidi Luiz akasababisha penalti mbili, moja nusura iigharimu Juve pointi zote tatu katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya RB Leipzig, na nyingine katika dakika za mwisho nyumbani katika Serie A dhidi ya Cagliari alipowazadia wageni sare ya 1-1.
Alisha amefunga mabao mawili katika mechi zake 11 za kwanza Serie A akiwa na Juve, lakini mechi sita kaingia kutokea benchini. Ni mwanzo wa giza kwa wote wakikaa benchini.