Arsenal yaifuata Sporting CP robo fainali UEFA
Muktasari:
- Arsenal sasa itakutana na Sporting CP katika hatua ya robo fainali, baada ya timu hiyo ya Ureno kufanya comeback ya kusisimua kutoka nyuma kwa jumla ya mabao 3-0 ilipofungwa ugenini na kushinda 5-0 nyumbani dhidi ya Bodo/Glimt.
MABAO kutoka kwa Eberechi Eze na Declan Rice, yameisaidia Arsenal kupata ushindi wa 2-0 nyumbani dhidi ya Bayer Leverkusen na kufuzu hatua ya robo fainali ya UEFA Champions League.
Arsenal sasa itakutana na Sporting CP katika hatua ya robo fainali, baada ya timu hiyo ya Ureno kufanya comeback ya kusisimua kutoka nyuma kwa jumla ya mabao 3-0 ilipofungwa ugenini na kushinda 5-0 nyumbani dhidi ya Bodo/Glimt.
Arsenal iliingia kwenye mechi hii iliyochezwa Emirates usiku wa Jumanne Machi 17, 2026 ikiwa sare na timu hiyo ya Ujerumani, baada ya penalti ya dakika za mwisho ya Kai Havertz wiki iliyopita kuifanya mechi ya kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1, na hawakuipa Leverkusen nafasi ya kutulia katika kipindi cha kwanza.
Arsenal ilikaribia kufunga mara mbili kupitia Gabriel Magalhães kwa mipira ya kona, lakini kipa wa Leverkusen, Janis Blaswich alifanya sevu nzuri kuzuia nyavu zisitikiswe.
Hata hivyo, hakuweza kuzuia bao la kwanza, ambapo Eze aliutuliza mpira nje kidogo ya eneo la hatari, akajigeuza na kupiga shuti kali lililoingia wavuni juu, likiwa bao lake la kwanza kwenye Champions League.
Arsenal iliendelea na kasi hiyo kipindi cha pili, na Rice akahitimisha ushindi huo baada ya kuukimbilia mpira uliotolewa na Leverkusen na kuupiga kwa utulivu kuingia kona ya chini ya lango.
Baada ya kuhakikisha ushindi, kocha Mikel Arteta alipata nafasi ya kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wake muhimu kabla ya Arsenal kukutana na Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup itakayochezwa Wembley, Jumapili hii Machi 22, 2026.