Joshua anarudi tena ulingoni
Muktasari:
- Joshua alirejea kwa kishindo ulingoni baada ya kumchapa Paul katika raundi ya sita ya pambano lao la uzani wa juu lililofanyika Miami, Florida, Ijumaa ya wiki iliyopita.
LONDON, ENGLAND: BONDIA kutoka England, Anthony Joshua amepewa ofa ya kupigania taji la dunia siku chache tu baada ya ushindi wake wa KO katika pambano dhidi ya Jake Paul.
Joshua alirejea kwa kishindo ulingoni baada ya kumchapa Paul katika raundi ya sita ya pambano lao la uzani wa juu lililofanyika Miami, Florida, Ijumaa ya wiki iliyopita.
Mbabe huyu alimpiga Paul ngumi kali kwa mkono wa kulia iliyomwangusha chini na akashindwa kusimama kabla ya mwamuzi hajamaliza kumhesabia hadi 10.
Hilo lilikuwa ni pambano la kwanza la AJ tangu alipochapwa kwa KO dhidi ya Daniel Dubois katika pambano la uzito wa juu la IBF lililofanyika katika Uwanja wa Wembley mwaka jana.
Sasa baada ya pambano hilo, Promota wa Matchroom, Eddie Hearn anayemsimamia Joshua, inaripotiwa anapanga pambano jingine la bondia huyo, linaloweza kufanyika kati ya Februari au Machi mwakani.
Pambano hilo la mwanzoni mwa mwaka 2026 linadaiwa litatumika kama sehemu ya maandalizi ya pambano litakalofanyika mwisho mwa mwaka ujao kati ya bondia huyo dhidi ya Tyson Fury, ambaye anatarajiwa kurejea katika mchezo huo mwakani licha ya kutangaza kustaafu hapo awali baada ya kupoteza mbele ya Oleksandr Usyk.
Inaelezwa pambano la kati ya Februari hadi Machi linaweza kuwa kati ya Joshua dhidi ya bingwa wa dunia wa WBO uzani wa juu, Fabio Wardley.
Wardley alishinda taji la muda la dunia la WBO uzani wa juu baada ya kumchapa Joseph Parker Oktoba, kabla ya kupandishwa hadhi na kuwa bingwa kamili baada ya Oleksandr Usyk kuuachia mkanda huo.
Bosi wa Queensberry, Frank Warren ambaye pia ni promota wa Fury, aliwataja Moses Itauma na Wardley kama mabondia ambao Joshua anatakiwa apigane nao kwa sasa ikiwa anahitaji kurudisha mkanda wa ubingwa wa dunia.
Alipoulizwa kama yuko tayari kufanikisha pambano kati ya Wardley na Joshua, Warren alijibu: “Ikiwa Joshua atakubali bila shaka nitafanya hivyo, nitaenda nyumbani kwake siku ya Krismasi. Nitaenda pale na tutakamilisha makubaliano. Hilo ni pambano la taji la dunia. Unataka kupigania taji la dunia, pigana na Fabio Wardley.”