Jamie Vardy hana bahati, ashuka tena na Cremonese
Muktasari:
- Vardy alishuka na Leicester hadi EFL Championship na kisha kuondoka England kwa ‘machungu’ na kuhamia Serie A kwa matumaini ya kupata ukurasa mpya wa mafanikio kabla ya kujikuta akishuka tena daraja na Cremonese.
Baada ya kushuka na Leicester City msimu wa 2024/25, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya England, Jamie Vardy anaendelea kupitia kipindi kigumu kisicho na bahati baada ya kushuka daraja misimu wa pili mfululizo akiwa na Cremonese ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A
Vardy alishuka na Leicester hadi EFL Championship na kisha kuondoka England kwa ‘machungu’ na kuhamia Serie A kwa matumaini ya kupata ukurasa mpya wa mafanikio kabla ya kujikuta akishuka tena daraja na Cremonese.
Hata hivyo, mambo yameenda kinyume na matarajio baada ya timu hiyo kuporomoka rasmi kutoka Serie A kwenda Serie B msimu huu wa 2025/2026, kutokana na matokeo mabaya katika mechi za lala salama.
Kama hiyo haitoshi, makali ya ufungaji ya mshindi huyo wa zamani wa kiatu cha dhahabu Ligi Kuu England yameonekana kufifia kwa kiasi kikubwa kwani amefunga mabao saba pekee msimu mzima.
Licha ya kupambana na kufunga mabao muhimu katika mechi ya mwisho kujaribu kuiokoa timu hiyo, bahati haikuwa upande wake na kujikuta yakimtokea kama ilivyokuwa England kwa timu kushuka daraja.
Verdy, 39, sasa ameacha maswali kwa mashabiki wengi wa soka, ikiwa huu ndiyo mwisho wa zama zake katika soka la ushindani ama bado ana nguvu za kupambana msimu ujao 2026/27.
Nyota huyo aliisaidia Leicester City aliyojiunga nayo mwaka 2012 kubeba taji la Ligi Kuu England msimu wa 2015/16, akifunga mabao 24 katika mechi 36.
Kwa sasa kuna tetesi nyota huyo ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo wenye kipengele cha kuongeza mmoja, inatajwa huenda akarejea England kujiunga na timu yake ya zamani ya nyumbani alikoanzia maisha ya soka, Sheffield Wednesday ambayo msimu ujao itacheza EFL League One baada ya kushuka daraja kutoka Championship.