Imeisha hiyoo! Mo Salah akichomoa, vichwa hivi vinakuja Anfield

Muktasari:

MAMBO mazito. Supastaa, Mohamed Salah anazidi kuiweka Liverpool njiapanda.

LIVERPOOL, ENGLAND. MAMBO mazito. Supastaa, Mohamed Salah anazidi kuiweka Liverpool njiapanda.

Staa huyo wa kimataifa wa Misri, Mo Salah, 29, amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake wenye thamani ya Pauni 200,000 kwa wiki, ameripotiwa kwamba anataka alipwe mshahara mkubwa kwelikweli ili aendelee kubaki Anfield.

Salah anatajwa kama mwanasoka bora kabisa duniani kwa sasa. Na kutokana na Kylian Mbappe kupiga hesabu za kuachana na Paris Saint-Germain kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwakani, miamba hiyo ya Ufaransa inatafuta mtu wa kuja kuziba pengo lake, huku wakimtazama Mo Salah kuwa mtu mwafaka wa kwenda kuchukua mikoba.

Real Madrid nao kwa muda mrefu wamekuwa wakimsaka Mo Salah kwenda akakipige huko Santiago Bernabeu.

Akiwa na umri wa miaka 29, staa huyo anadhani ni wakati wake wa kunasa dili la pesa ndefu kabla ya kufikia mwisho wa maisha yake ya soka. Shida ni kwamba Liverpool haina uwezo wa kumlipa Mo Salah mshahara anaotaka, kama ilivyofanya Manchester United kwa Alexis Sanchez ilipokuwa ikimlipa Pauni 505,000 kwa wiki. Miamba hiyo ya Anfield inaweza kujitutumua na kumlipa Mo Salah mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki.

Kutokana na hilo, Liverpool imeripotiwa kwamba huenda ikageuza macho kwa mastaa hawa watano kunasa saini zao kuchukua mikoba ya Mo Salah kama watashindwa kufikia makubaliano kwenye ishu ya mkataba mpya.

Mchezaji wa kwanza ni Kylian Mbappe. Supastaa huyo Mfaransa, mwenye umri wa miaka 22 tu, alishaweka wazi anaachana na PSG. Real Madrid kwa muda mrefu imekuwa ikimtaka staa huyo wa zamani wa Monaco, huku Mbappe mwenyewe akiwa anaishabiki Los Blancos tangu utoto wake. Hata hivyo, Real Madrid wapo njiapanda, wamchukue nani, Mbappe au Erling Haaland. Jambo hilo linawafanya Liverpool kuwa na nafasi kwa Mbappe, ambaye huko nyuma aliwahi kuweka wazi kuvutiwa na kocha Jurgen Klopp.

Mchezaji wa pili ni Ousmane Dembele. Umri wake ndio kwanza miaka 24, na staa huyo Mfaransa ni mchezaji mahiri kwelikweli, shida ni majeruhi tu yamekuwa yakimwaandama na. Fowadi huyo alikuwa moto kwelikweli Borussia Dortmund na hapo kuwafanya Barcelona kushawishika kulipa Pauni 138 milioni kunasa saini yake.

Kwa sasa Barcelona wapo tayari kumfungulia milango ya kutoka Dembele, jambo ambalo Liverpool wanaweza kufanya haraka kwenda kunasa saini yake,.

Mchezaji wa tatu ni Marco Asensio. Staa mwingine mwenye kipaji cha hali ya juu kabisa, Asensio bado hajapewa nafasi ya kutosha ya kuonyesha ubora wake wa uwanjani huko Bernabeu. Amecheza mechi 135 za ligi tangu 2015.

Mchezaji wa nne ni Dusan Vlahovic. Fowadi huyo wa Fiorentina amekuwa maarufu sana huko Ulaya kwa sasa akiwindwa na klabu kubwa kibao. Vlahovic, 21, mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao na ameshakataa ofa ya kubaki. Vlahovic ana kimo cha futi 6 na inchi 3, hivyo kama atatua Anfield jambo hilo litamfanya Diogo Jota, ahamishiwe pembeni ili kati apangwe staa huyo mwenye kimo kirefu kuzitendea haki krosi za kina Trent Alexander-Arnold na Andrew Robertson.

Mchezaji wa tano ni Philippe Coutinho. Liverpool wanaweza kufanya uamuzi wa kumrudisha ‘Mchawi Mdogo’ kwenye kikosi chao.