Ilibaki kiduchu Gallagher atue Man United
Muktasari:
- Man United iliwasiliana na klabu ya Atletico Madrid kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo Mwingereza kwa mkopo.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imekwama kwenye dakika za mwisho kabisa kunasa huduma ya kiungo Conor Gallagher wakati dirisha la usajili lilipofungwa Jumatatu.
Man United iliwasiliana na klabu ya Atletico Madrid kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo Mwingereza kwa mkopo.
Lakini, miamba hiyo ya La Liga iliwaambia mabosi wa Man United kwamba wao wanachotaka ni kumpiga bei jumla kiungo huyo wa zamani wa Chelsea na si kumtoa kwa mkopo. Na kutokana na hilo, Man United iliamua kufuta mpango huo wa kusajili kiungo na hivyo itasubiri kwenye dirisha la Januari au lile la mwisho wa msimu.
Man United ilikwama pia kwenye mpango wao wa kunasa huduma ya kiungo mkabaji wa Brighton, Carlos Baleba kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Hilo limetokana na Brighton kuhitaji ada inayozidi Pauni 100 milioni ili kuachana na mkali huyo wa Camerooni.
Bruno Fernandes na Casemiro wamekuwa machaguo ya kocha Ruben Amorim kwenye safu ya kiungo msimu huu huku Kobbie Mainoo na Manuel Ugarte wakisubiria kutokea benchini.
Man United eneo ambalo iliweka kipaumbele kikubwa kwenye dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ni kwenye fowadi na ndiyo maana imetumia Pauni 200 milioni kunasa huduma za mastaa Matheus Cunha kutoka Wolves, Bryan Mbeumo kutoka Brentford na Benjamin Sesko kutoka RB Leipzig.
Kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, Man United ilinasa huduma ya kipa mpya, Senne Lammens kutoka Royal Antwerp kwa ada ya Pauni 18.2 milioni.
Man United imeanza msimu kwa kuwa na matatizo kwenye goli lake kutokana na makipa Altay Bayindir na Andre Onana kushindwa kuonyesha viwango bora, kila mmoja akiruhusu mabao ya kizembe na kuigharimu timu hiyo kwenye mechi zake nne zilizocheza, tatu kwenye Ligi Kuu England na moja kwenye Kombe la Ligi, ambako ilitupwa nje na timu ndogo, Grimsby.