Ibrahima Konate anakaribia kusaini mkataba mpya Liverpool
Muktasari:
- Liverpool imekuwa ikipambana usiku na mchana kuhakikisha fundi huyu anakubali kusaini na kuendelea kusalia nao baada ya kuwepo kwa tetesi anaweza akatimkia Real Madrid.
BEKI kisiki wa Liverpool na timu ya taifa ya Ufaransa Ibrahima Konate, mwenye umri wa miaka 26, ambaye anatarajia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu huu, kuna uwezekano mkubwa akasaini mkataba mpya katika wiki chache zijazo.
Liverpool imekuwa ikipambana usiku na mchana kuhakikisha fundi huyu anakubali kusaini na kuendelea kusalia nao baada ya kuwepo kwa tetesi anaweza akatimkia Real Madrid.
Tovuti ya Football Insider Novemba mwaka huu ilifichua Liverpool ilikuwa tayari kuharakisha mipango yao ya kutafuta mbadala wa Konate msimu ujao, lakini sasa wameachana na mpango huo, badala yake wanapambana kuhakikisha inamsainisha mkataba mpya beki huyo.
Miezi kadhaa iliyopita ilielezwa Liverpool ingekuwa tayari kupokea Pauni 15 milioni kama ada ya uhamisho kwa timu itakayohitaji huduma ya Konate lakini hiyo ilikuwa ni kwa sababu waliona hakuna uwezekano wa kumsainisha mkataba mpya.
Tangu kuanza kwa msimu huu Konata amecheza mechi 22 za michuano yote.
Joshua Zirkzee
AS Roma imefungua rasmi mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24. Kwa mujibu wa taarifa, Roma inataka kumsajili Zirkzee kwa mkataba wa mkopo wa nusu msimu, utakaokuwa na kipengele cha kumnunua mazima kwa Pauni 30 milioni ikiwa itaridhishwa na kiwango chake. Zirkzee alionyesha kiwango bora akiwa na Bologna lakini tangu ajiunge na Man United mambo yanaonekana kuwa magumu kwake.
Sergio Ramos
MANCHESTER United inatafuta beki mwenye uzoefu kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ulizi na miongoni mwa majina yaliyopo katika orodha yao ni la nyota wa zamani wa Real Madrid, Sergio Ramos, 39 ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Monterrey ya Mexico. Ikiwa makubaliano yatafikiwa Ramos anaweza akasainishwa mkataba wa mwaka mmoja na mshahara wake unadaiwa utakuwa chini ya Pauni 100,000 kwa wiki.
Matteo Guendouzi
SUNDERLAND imemweka kwenye rada zao kiungo wa zamani wa Arsenal, Matteo Guendouzi, 26, anayekipiga Lazio ya Italia. Inaelezwa Sunderland imewasilisha ofa ya Pauni 21.4 milioni ili kumpata staa huyo wa Ufaransa ambaye ana uzoefu wa ligi ya England kutokana na kuwahi kupita Arsenal kuanzia mwaka 2020 hadi 2022. Msimu huu amecheza mechi 13 za michuano yote na kufunga mabao mawili.
Oxlade-Chamberlain
KIUNGO wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Alex Oxlade-Chamberlain, 32, anataka kurudi England dirisha lijalo la usajili la majira ya baridi kama mchezaji huru baada ya kuachana na Besiktas Agosti mwaka huu. Fundi huyu ambaye pia aliwahi kupita Liverpool, amekuwa na changamoto ya majeraha ya mara kwa mara hali iliyosababisha kuwa nje ya Uwanja kwa muda mrefu.
Ivan Toney
MSHAMBULIAJI wa Al Ahli ya Saudi Arabia,Ivan Toney, 29, anaonekana hana mpango wa kuondoka katika klabu hiyo Januari mwakani licha ya timu kadhaa za Ligi Kuu England kutaka kumsajili. Inaelezwa sababu kubwa ni masuala ya kodi ambayo yatasababisha apoteze kiasi kikubwa cha mshahara wake hata kama akisaini mkataba wa mkopo. Chelsea, Manchester United na West Ham zinahusishwa kumhitaji.
Promise David
WEST Ham United imepata pigo katika mpango wao wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Canada Promise David, 24, anayeichezea Union Saint-Gilloise ya Ubelgiji. Inaelezwa mpango huo umefeli kwa sababu mchezaji huyo hataki kuacha kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kujiunga na timu inayopambana kuepuka kushuka daraja licha ya ofa nono aliyopata.
Adama Traore
WOLVES inafikiria kufanya usajili dirisha la Januari kwa kumrudisha winga wao wa zamani ambaye kwa sasa anaichezea Fulham, Adama Traore, 29. Traore ambaye aliwahi kucheza Wolves mwaka 2018 hadi 2023, hajaonyesha kiwango bora tangu ajiunge na Fulham na tangu kuanza kwa msimu huu hadi sasa amecheza mechi 13 za michuano yote na kutoa asisti moja.