Huyo Baleba kaomba kwenda Man United
Muktasari:
- Wakati Baleba akifikisha maombi hayo kwa mabosi wa timu yake, wakala wa mchezaji huyo amekuwa bize naye kupamba dili hilo litokee baada ya kufikia makubaliano ya maslahi binafsi na Man United.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Kiungo mkata umeme, Carlos Baleba ameripotiwa kuwasilisha maombi yake ya mdomo kwa mabosi wa Brighton akiwaomba wamfungulie mlango wa kwenda kujiunga na Manchester United.
Wakati Baleba akifikisha maombi hayo kwa mabosi wa timu yake, wakala wa mchezaji huyo amekuwa bize naye kupamba dili hilo litokee baada ya kufikia makubaliano ya maslahi binafsi na Man United.
Man United akili yao kwa sasa ipo kwenye kukamilisha dili la kiungo huyo baada ya kumalizana na tatizo la ushambuliaji. Miamba hiyo ya Old Trafford dirisha hili limewasajili washambuliaji Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko, ambao wataongoza safu ya wakali watatu kwenye fowadi katika mtindo wa uchezaji wa Kocha Ruben Amorim wa 3-4-3.
Wakati ikiwa bado makubaliano kati ya Man United na Brighton hayajafikiwa, mchezaji huyo mwenyewe yupo tayari kwenda kukipiga Old Trafford.
Baleba ameripotiwa kufikia makubaliano ya mdomo na mabosi wa Brighton ili kumruhusu kwenda Man United. Wakala wa mchezaji huyo pia amekubali baada ya kuvutiwa na ofa ya makubaliano binafsi ya mchezaji.
Kinachoelezwa ni Brighton huenda ikaendelea kung'ang'ania kulipwa ada ya Pauni 100 milioni kwenye uhamisho huo, kitu ambacho Man United haitakuwa ana tatizo kwao kama timu ya Baleba itakubali kumuuza kwa sasa.
Man United inatarajia kuvuna pesa kwa kuwaachia Alejandro Garnacho, Jadon Sancho, Antony na Tyrell Malacia, hivyo kuwa na nafasi ya kumsajili Baleba.
Man United inafahamu wazi ikishindwa kumsajili Baleba kwenye dirisha hili, thamani yake itazidi kupanda, wakati sasa thamani yake ikitajwa kuwa Pauni 100 milioni. Kinachoelezwa ni Brighton inataka Baleba aondoke kwa pesa kama ambayo walimuuza Moises Caicedo kwenda Chelsea, Pauni 115 milioni. Brighton imekuwa na kawaida ya kuwauza pesa nyingi mastaa wake, akiwamo Alexis Mac Allister (Pauni 55 milion), Marc Cucurella (Pauni 56 milioni) na Robert Sanchez (Pauni 25 milioni) kwa kuwataja kwa uchache.