Hugo Ekitike kufosi dili la Liverpool
Muktasari:
- Staa huyo Mfaransa amewekwa kipaumbele kwenye mipango ya usajili wa Liverpool katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuona mpango wa kumsajili straika wa Newcastle United, Alexander Isak, utawagharimu pesa nyingi, karibu Pauni 125 milioni.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA, anayesakwa kwa nguvu zote na Liverpool, Hugo Ekitike ameripotiwa kuiandikia Eintracht Frankfurt barua ya kuomba kuondoka ili kukamilisha ndoto zake za kwenda kukipiga huko Anfield.
Staa huyo Mfaransa amewekwa kipaumbele kwenye mipango ya usajili wa Liverpool katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuona mpango wa kumsajili straika wa Newcastle United, Alexander Isak, utawagharimu pesa nyingi, karibu Pauni 125 milioni.
Kuona hilo, Liverpool imeamua kuhamishia nguvu kwa Ekitike, ambaye anawapa uhakika kwamba wanaweza kumpata kutokana na mchezaji mwenyewe kuvutiwa na mpango wa kwenda kukipiga kwenye kikosi cha Arne Slot.
Liverpool italazimika kulipa pesa iliyotajwa kwenye kipengele cha mkataba wa Ekitike ili kunasa saini yake, ambapo inatajwa kuwa ni Pauni 86.5 milioni, ambayo ni nafuu kulinganisha na ada ya uhamisho ya Isak.
Na kinachoripotiwa, Ekitike amewasilisha maombi ya kutaka kuhama Frankfurt.
Kwa mujibu wa Sport Bild, Ekitike yupo tayari kulazimisha uhamisho huo ili utokee. Newcastle ilikuwa na matumaini ya kumsajili Ekitike ili akacheze pamoja na Isak, lakini Liverpool sasa inaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kunasa huduma yake.
Kocha Slot bado ana utajiri mkubwa wa wachezaji kwenye safu ya ushambuliaji akiwa na wakali Mohamed Salah, Luis Diaz, Cody Gakpo, Darwin Nunez na Federico Chiesa.
Lakini, anataka kumpunguzia Mo Salah mzigo wa kulazimika kufunga mabao na kuja kuongeza ushindani wa nafasi kwenye safu ya ushambuliaji.
Liverpool inaonekana kuhitaji kulinda safu yao hiyo iwe kamili baada ya kukataa ofa ya Bayern Munich ya Pauni 58.6 milioni inayomhusu Luis Diaz.
Hadi sasa, Liverpool imeshakamilisha usajili wa mastaa sita, ikiwamo Jeremie Frimpong, Milos Kerkez na Florian Wirtz ambaye uhamisho wake umevunja rekodi ya usajili huko England, ilipomnasa kwa pesa ndefu, Pauni 116.5 milioni.