Hojlund, Rashford wamtumia ujumbe mzito Amorim
Muktasari:
- Miongoni mwa wachezaji hao ni Rasmus Hojlund, ambaye Kevin De Bruyne amemlinganisha na Erling Haaland, baada ya Mdenmark huyo kuibuka shujaa wa Napoli katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
WAKATI Manchester United ikiwa haina mwanzo mzuri msimu huu, nyota waliokosa nafasi kikosini hapo na kuondoka, wanakiwasha ipasavyo klabu zingine, huku usiku wa kuamkia leo wakifanya balaa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kufanya vizuri kwa nyota hao, ni ujumbe tosha kwa kocha mkuu wa Man United, Rasmus Hojlund ambaye amehusika moja kwa moja kuondoka kwao.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Rasmus Hojlund, ambaye Kevin De Bruyne amemlinganisha na Erling Haaland, baada ya Mdenmark huyo kuibuka shujaa wa Napoli katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Manchester United hawakufuzu michuano hiyo baada ya kupoteza fainali ya Europa League msimu uliopita dhidi ya Tottenham, lakini wachezaji kadhaa waliokosa nafasi katika klabu hiyo walikuwa uwanjani Jumatano usiku wakicheza kwa kiwango kikubwa.
Hojlund, ambaye mwanzoni mwa msimu aliondolewa kwenye kikosi cha Ruben Amorim, ameendelea kung’ara tangu ajiunge na mabingwa wa Italia, Napoli. Amefunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Sporting Lisbon na kutajwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Bao la kwanza alilifunga dakika ya 36 akimalizia pasi safi ya De Bruyne, kabla ya Sporting kusawazisha kwa penalti kipindi cha pili. Hata hivyo, ushirikiano kati ya De Bruyne na Hojlund ulirejesha uongozi wa Napoli baada ya Mbelgiji huyo kupiga krosi iliyompatia Mdenmark nafasi ya kufunga kwa kichwa.
"Umekuwa ni usiku niliokuwa ninauota, kucheza Ligi ya Mabingwa," amesema Hojlund baada ya mechi hiyo.
"Nilisherehekea kwa kugusa beji ya Napoli kwa sababu nina furaha kucheza hapa, na pia beji ya Ligi ya Mabingwa kwa sababu napenda kufunga Ulaya."
De Bruyne amempongeza Hojlund akimlinganisha na Haaland, huku akibainisha maeneo ambayo bado anaweza kuboresha.
"Tulistahili ushindi. Nilikuwa natafuta nafasi sahihi kumpasia Rasmus na alifanya kilichobaki. Nafikiri anafanana sana na Haaland, wote wanapenda kushambulia. Labda Hojlund hupenda pia kushuka kucheza mpira, lakini anatakiwa kushambulia mara nyingi zaidi kwa sababu anaweza kufunga na kutusaidia sana," amesema De Bruyne.
Kauli hiyo ya De Bruyne inafanana na aliyowahi kusema kocha wa zamani wa Atalanta, Gian Piero Gasperini, kabla ya Hojlund kuhamia Man United kwa Pauni 72 milioni mwaka 2023. Hadi sasa, Hojlund amefunga mabao matatu katika mechi tano za kwanza tangu kutua Napoli kwa mkopo wenye nafasi ya kununuliwa kwa Pauni 38 milioni.
Hojlund hakuwa pekee mchezaji aliyetoka Man United kwa kukosa nafasi na kwenda kuuwasha usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana. Anthony Elanga na Marcel Sabitzer pia walitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi, huku Marcus Rashford akitoa pasi ya bao la Barcelona dhidi ya PSG.
Rashford alipiga krosi safi iliyomwezesha Ferran Torres kufunga bao la kuongoza kwa Barca, ingawa PSG ilipindua matokeo na kushinda 2-1 kupitia mabao ya Senny Mayulu na Gonçalo Ramos. Rashford sasa amehusika na mabao katika mechi tano kati ya sita alizochezea Barcelona, ikiwa ni pamoja na mabao mawili ya ushindi dhidi ya Newcastle katika mechi ya kwanza ya makundi.
Elanga, ambaye aliachwa na Man United mwaka 2023 na kuhamia Nottingham Forest kwa Pauni milioni 15 kabla ya kuuzwa Newcastle kwa Pauni milioni 55, aliendelea kung’ara kwa kuchangia mabao mawili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Union Saint-Gilloise.
Sabitzer naye ameibuka nyota katika ushindi mnono wa RB Leipzig, akitoa msaada kwa bao la nne la timu hiyo.
Wote Elanga na Sabitzer waliondoka United kabla ya ujio wa Sir Jim Ratcliffe na INEOS, lakini mafanikio yao yanaibua kumbukumbu ya vipaji vilivyoshindwa kung’ara ndani ya Old Trafford.
Manchester United haina mwendo mzuri kwenye Premier msimu huu ikishika nafasi ya 14 baada ya michezo sita, ikishinda miwili pekee, sare moja na kupoteza mitatu. Matokeo hayo yameongeza presha kwa kocha Ruben Amorim kabla ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Sunderland pale Old Trafford.