Hofu ya nyoka wenye sumu yatikisa kambi Kombe la Dunia
Muktasari:
- Wachezaji kutoka Ujerumani, Uswisi na Norway wanasema wanaogopa kukutana uso kwa uso na wanyama hao wa porini, hasa nyoka aina ya copperhead ambao ni wa sumu na hupatikana sana katika Jimbo la North Carolina, Marekani.
WINSTON-SALEM, MAREKANI: NAHODHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joshua Kimmich na wachezaji wengine wanaoshiriki Kombe la Dunia, wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu uwepo wa nyoka wenye sumu kali katika maeneo wanayoishi wakati wa michuano hiyo.
Wachezaji kutoka Ujerumani, Uswisi na Norway wanasema wanaogopa kukutana uso kwa uso na wanyama hao wa porini, hasa nyoka aina ya copperhead ambao ni wa sumu na hupatikana sana katika Jimbo la North Carolina, Marekani.
Kimmich na wachezaji wenzake waliripotiwa kukutana na nyoka huyo katika kambi yao ya mazoezi huko Winston-Salem, huku timu ya Uswisi ikiweka alama eneo fulani la nje ya kambi yao iliyopo mji wa San Diego ulioko kusini mwa jimbo la California, Marekani kama 'Eneo la nyoka', kabla ya michuano hiyo.
Kimmich anasema waliona nyoka na wakaambiwa ni wa sumu kali na ikiwa utang'atwa kuna uwezekano mkubwa ukapelekwa hospitalini kwa sababu ni hatari na ni miongoni mwa wanyama ambao hawajawahi kukutana nao.
Nyota huyo anasema hali hiyo ni ya hatari zaidi kwao na wanapaswa kuongeza umakini, kwa sababu kwao Ujerumani hakuna vitisho vikubwa vya wanyama pori hatari kama ilivyokuwa Marekani inapofanyika michuano hiyo kwa kushirikiana na Canada na Mexico.
Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia, wana aina chache za nyoka na ni wachache tu wenye sumu, jambo linalowatisha nyota hao kutokana na mazingira magumu wanayokutana nayo kwa sasa Marekani.
Kwa upande wa nahodha wa Norway, Kristian Thorstvedt anasema hakuwa na furaha tangu aliposikia uwepo wa wanyama hao hatari katika Jimbo la North Carolina, Jambo linaloonyesha wasiwasi mkubwa wa kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Dunia.