Prime
Hii vesti kiboko ya wachezaji wavivu

Muktasari:
- Hapo ndipo ilipoibuka kivazi chenye mwonekano kama wa vesti, ambayo mchezaji anavalishwa kwenye mazoezi au mechi kutambua kiwango chake cha uwangani.
LONDON, ENGLAND: KWENYE soka la kisasa, mchezaji anaposajiliwa kutoka timu moja kwenda nyingine, kuna vitu vingi vinazingatiwa. Ipo hivi, baada ya skauti wa timu A kumwona mchezaji wa timu B na kuvutiwa naye, kwamba wanataka akajiunge na timu A, kuna taratibu nyingi zinafuatwa, lakini timu A kabla ya kunasa saini ya mchezaji huyo, itahitaji uwezo wake wa uwanjani.
Kwenye hilo la kufahamu uwezo wa uwanjani, ndipo teknolojia inapotumika kwenye soka la kisasa. Kwa sasa, timu haitahitaji kutuma skauti wake kwenye kila mechi atakayocheza mchezaji huyo kujua kiwango chake cha uwanjani, bali zinaweza kutumia taarifa za mchezaji huyo zinazohusu kiwango chake ambazo zimekuwa zikirekodiwa kwenye mechi hadi katika mazoezi anayofanya. Kwamba anafaa au hafai. Anapiga kazi au ni mvivu uwanjani?
Hapo ndipo ilipoibuka kivazi chenye mwonekano kama wa vesti, ambayo mchezaji anavalishwa kwenye mazoezi au mechi kutambua kiwango chake cha uwangani.

Kivazi hicho, ni mapinduzi ya kisayansi, ambapo kinawekwa kifaa maalumu cha kurekodi mikimbio yote ya mchezaji ndani ya uwanja, amecheza eneo la ukubwa gani la uwanjani, amekimbia kwa umbali gani ili kufahamu utimamu wake ndani ya uwanja.
Kifaa hicho (GPS) kilichochomekwa sehemu ya nyuma kwenye vesti hiyo, ambapo mchezaji akivaa itakuwa sehemu ya juu ya mgongo wake, taarifa zote itakazorekodi za kuhusu mchezaji huyo kwa muda wake aliokuwa ndani ya uwanja, inatuma taarifa hizo kwenye simu au kompyuta ambayo imeunganishwa moja kwa moja kwa ajili ya kupokea taarifa hizo.
Sasa kwenye soka la kisasa, taarifa za kifaa hicho hutumika pia kwenye kuipa timu A nguvu ya kufanya usajili wa mchezaji wa kutoka B waliyevutiwa naye.

Vesti yenyewe
Vesti hiyo imetengenezwa kwa ukubwa tofauti na kwa maana hiyo, hata bei yake pia inatofautiana. Kwa kile cha STATSports APEX Athlete Series Football GPS Tracker, bei yake ni kati ya Pauni 169.99 na Pauni 199.99 kulingana na ukubwa wake.
Teknolojia yake inatotumika ni ios, Android huku ukubwa wa chipu yake ni ukubwa wa 8 GB, huku ikitengenezwa kwa malighafi nyepesi sana huku betri yake ikiwa na nguvu ya 1000 Milliamp Hours. Namna kinavyotuma taarifa yake ni kupitia Bluetooth. GPS iliyowekwa ni ya umbo la mstatili na ina uwezo wa kutumia taarifa kwenye skrini yenye ukubwa wa inchi 33. Shirikisho la soka la kimataifa la vyama vya soka (Fifa) limepitisha matumizi ya kifaa hicho kwa wanasoka duniani.

Kinachopimwa kwa mchezaji
Katika kuhakikisha mchezaji anafanya kila kinachohitajika ndani ya uwanja na kuboresha ubora wake wa mchezaji, anapovalishwa vesti hiyo, itapima vitu 16, lakini vikubwa ni kasi, umbali, eneo alilocheza muda mwingi (Heatmaps), data na vinginevyo. Kwenye soka la kisasa, imekuwa kawaida ya mashabiki wanaotazama kupitia televisheni, kuona takwimu za mchezaji kwamba amekimbia kilomita ngapi uwanjani, au amecheza eneo gani zaidi, basi taarifa hizo zinapatikana kwa mchezaji aliyevalishwa vesti hiyo.

Kwa maana hiyo, ni rahisi kuona mchango wa mchezaji ndani ya uwanja kama alikuwa mvivu au alipiga kazi ya maana kwa kuangaliwa kilomita ngapi amekimbia uwanjani. Benchi la ufundi litatumia takwimu hizo kuboresha kiwango cha mchezaji.

Kwa kuzingatia kiwango cha mchezaji ndani ya uwanja, kifaa hicho kitatoa tathmini pia ya mchezaji husika kuwa amechoka kulingana na takwimu zake zitakazokusanywa kwenye mechi kadhaa atakazokuwa amecheza, hivyo itasaidia timu kumpumzisha mchezaji ili kumwondoa kwenye hatari ya kupata majeraha. Timu kubwa karibu zote kwenye soka la dunia kwenye kikosi chake kuna vesti hizo kwa ajili ya kupima viwango vya wachezaji wao.