Hazard! Anaisha na haya...

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MADRID, HISPANIA. ILIKUWA mwaka 2019, wakati bilionea Roman Abramovic alipokubali yaishe mbele ya Florentino Perez na kukubali kuchukua Euro 115 milioni kwa ajiili ya kumuuza Eden Hazard kujiunga na matajiri hao wa Hispania.

Katika kipindi hiki  Hazard alikuwa ametoka kuwapa Chelsea  kombe la FA na Europa League, mashabiki wengi waliumia lakini mapenzi yao na staa huyo ndio yalisababisha yakubaliane na uhalisia kwamba Hazard alikuwa anaenda sehemu kubwa zaidi ambayo ilikuwa ni ndoto yake tangu aanze kucheza soka.

Maisha yameenda lakini Hazard kwa sasa anaonekana kuwa mzigo, licha yakuwa mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa zaidi kwenye kikosi cha Madrid akiwa anakunja zaidi ya Pauni 400,000 kwa wiki, staa huyu wa  kimataifa wa Ubelgiji ameshindwa kabisa kulipa kile kilichotarajiwa na wengi na hali hiyo huenda inawafanya mashabiki wa Chelsea kutabasamu badala ya kununa.
Hapa tumekuletea  takwimu za staa huyu tangu atue kwenye kikosi hiki cha Madrid na sababu ambazo zinatajwa kumuweka kwenye hali hii.


MAJERAHA
Wakati akiwa anaichezea Chelsea, licha ya ubora wake majeraha yalikuwa sehemu ya maisha yake lakini hakuwa anakaa sana nje kama ilivyo sasa.
Msimu wake wa kwanza akiwa na Madrid alicheza mechi 22 za michuano yote, akafunga bao moja na kutoa asisti saba.
Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba alikosa mechi 25 kutokana na majeraha mbali mbali ikiwa pamoja na kupasuka kwa mifupa ya vidole na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja.

Msimu wake wapili 2020/21 mambo yalikuwa mabaya zaidi kwani alicheza mechi 21 tu akifunga mabao manne na kutoa asisti moja huku muda mwingi akiutumia kwenye vitanda vya daktari kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona na maumivu ya misuli akikosa jumla ya mechi 42 za michuano yote hapa ni mjumuisho na zile za timu ya taifa ambapo alikosa mechi 12.

Msimu wa 2021/22 alicheza mechi 23 tu na hapo kwenye mechi 38 za La Liga alicheza 18 tu ambazo karibia zote aliingia akitokea benchi.
Hali ya kuaminika ilikuwa imeshaondoka kabisa na mbali ya majeraha ya kuvunjika mguu alisumbuliwa pia na abdominal influenza ambayo husababisha tumbo kuuma na kupata mafua.
Kimbembe  ni msimu huu kwani katika mechi 25 za  La Liga amecheza tatu tu na kwenye hizo 21 zilizobakia ni mechi tautu tu ndio alikuwa amekaa nje kwa majeraha lakini zilizobakia ni kwa sababu aliwekwa benchi kwa sababu Carlo Ancelotti hana imani naye.


KUTOKUELEWANA NA ANCELOTTI
Moja kati ya sababu zinazodaiwa kuchangia hali ya Hazard kutopata nafasi kubwa ya kucheza licha ya muda mwingine kuwa fiti hususani kwa msimu ni kutokuwepo kwa uhusiano mzuri baina yake na kocha wa sasa wa timu hiyo Carlo Ancelotti.
Kwa kinywa chake Hazard alithibitisha suala hili wakati anafanya mahojiano ya gazeti moja huko nchini Ubelgiji ambapo alisema:" Kuna heshima kati yetu, lakini siwezi kusema kwamba tunaongea kwa sababu kwa sasa hatuongei, lakini heshima lazima iwepo hata kama hanichezeshi natakiwa niheshimu mawazo ya mtu mkubwa kama huyu kutokana na kile ambacho amekifanya kwenye mpira wa miguu hadi sasa.


PRESHA YA VIATU VYA RONALDO
Wakati staa huyu anasajiliwa Madrid, ndio zilikuwa nyakati ambazo Cristiano Ronaldo anaondoka hapo na kujiunga na Juventus.
Lengo kubwa la kusajiliwa kwake ilikuwa ni kuziba pengo la Ronaldo kwa sababu ya kiwango alichokuwa anakionyesha kwa wakati huo na watu wengi waliamini kwamba angeliziba pengo.
 Presha ya kuthibitisha hilo ilimtafuna sana kiasi cha kutaka kuonyesha zaidi na mwisho akajikuta ameangukia kwenye wimbi la majeraha tofauti na ilivyokuwa Chelsea ambako hakuwa mtu anayelengwa sana hivyo hata namna ya uchezaji wake ilikuwa ni tofauti.
Hapa ilihitajika afunge ama atoe asisti ili kufikia matakwa ya mashabiki juu ya kuiona sura ya Ronaldo kwenye jezi yake.
 

TAKWIMU ZAKE
Tangu aanze maisha yake ya soka mwaka 2008 baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana ya Lille, staa huyu amecheza jumla ya mechi 620, akafunga mabao 167, asisti 156 ikiwa ni jumla ya dakika 44,419 na mechi nyingi alizocheza ni zile za Ligi Kuu England ambazo ni 245.
Vilevile kwa muda wote huo amechukua mataji 15  ambayo sita alichukua akiwa na Chelsea, EPL mawili, Europa mawili, FA moja na Carabao moja.
Saba amechukua akiwa na Madrid na mawili akiwa na Lille. Amechukua pia tuzo za mchezaji bora wa mwaka mara tatu mbili akiwa na Lille na moja akiwa na Chelsea.