HATIMAYE: Yadaiwa Messi yupo tayari sasa kucheza England

LIONEL MESSI
Muktasari:
Kutia chumvi katika uvumi huo, juzi Messi alifanya mahojiano maalumu na mwandishi maarufu wa habari za michezo nchini Hispania, Guillem Balague na alipoulizwa kuhusu kuondoka Barcelona hakukataa moja kwa moja suala hilo.
LONDON, ENGLAND
INASUBIRIWA kwa hamu na inadaiwa kuwa inaweza kutokea. Imeripotiwa kuwa staa wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi sasa yupo tayari kukipiga katika Ligi Kuu ya England.
Baada ya miaka 14 ya kukipiga katika timu moja na nchi moja, inadaiwa kuwa Messi mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa yupo tayari kujipima katika Ligi Kuu ya England huku klabu za Manchester United na Chelsea zikionyesha nia ya kumchukua.
Kwa mujibu wa Gazeti ya The Sun la Uingereza, klabu tatu za England zimeshafanya mawasiliano na wawakilishi wa Messi huku klabu moja kati ya hizo ikifanya mawasiliano mara mbili wiki iliyopita na kuonyesha dhamira thabiti ya kumchukua.
Kutia chumvi katika uvumi huo, juzi Messi alifanya mahojiano maalumu na mwandishi maarufu wa habari za michezo nchini Hispania, Guillem Balague na alipoulizwa kuhusu kuondoka Barcelona hakukataa moja kwa moja suala hilo.
“Sitaki kutazama mbali sana. Naishi kwa kipindi nilichopo na kwa sasa nipo Barcelona na katika Ligi Kuu Hispania ambapo naishi na kufanya vizuri,” alisema Messi akigoma kuzungumzia hali yake ya baadaye nchini humo.
Imeripotiwa kuwa mastaa kadhaa ambao ni marafiki wa Messi wanaocheza England wamemshawishi staa huyo ahamishie makali yake katika Ligi Kuu England huku utayari wa Messi kuhama Hispania ukichangiwa na matatizo yake ya masuala ya kodi nchini Hispania.
Messi na baba yake, Jorge Messi wanashtakiwa na mamlaka za Hispania kwa kosa la kukwepa kulipa kodi zinazofikia Pauni 3.1 milioni na tayari mwanasheria wa Serikali ya Hispania anayesimamia kesi hiyo anataka wawili hao wafungwe miezi 22 endapo watabainika na hatia katika kosa hilo.
Mkataba wa sasa wa Messi na Barcelona unatarajiwa kumalizika Juni 2018 na katika kipengele cha kuuzwa kwake ndani ya klabu hiyo ya Catalunya, klabu yoyote inayomtaka Messi italazimika kulipa dau la Euro 250 milioni kupata huduma yake.
Endapo atauzwa kwenda katika klabu yoyote kwa sasa, Messi anatarajiwa kuweka rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani akivunja rekodi inayoshikiliwa na staa wa Real Madrid, Gareth Bale ambaye aliuzwa kwa dau la Pauni 85 milioni kutoka Tottenham mwaka 2013.