Harry Kane ana jambo lake England

Muktasari:
- Kikosi cha kocha Xabi Alonso ndicho kilichomzuia Kane kupata taji lake la kwanza katika maisha yake ya soka wakati waliponyakua taji la Bundesliga msimu uliopita.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane amepiga mbili wakati Bayern Munich ikiichapa Bayer Leverkusen mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa mtoano kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano iliyopita.
Kikosi cha kocha Xabi Alonso ndicho kilichomzuia Kane kupata taji lake la kwanza katika maisha yake ya soka wakati waliponyakua taji la Bundesliga msimu uliopita.
Wakati ikisubiriwa mechi ya marudiano, Bayern ina uhakika mkubwa wa kupenya kwenye hatua hiyo na kutinga robo fainali, huku ikiongoza kwa tofauti ya pointi kwenye msimamo wa ligi, huku ikiwa na tofauti ya mabao tisa na mechi bado 10.
Na Bayern kwenye mechi zao zilizobaki, timu sita ni zile nane za chini, huku ni Mainz na RB Leipzig tu ndizo zilizopo kwenye sita za juu. Kane atakapotimiza ndoto zake za kushinda taji kubwa kwenye maisha yake ya soka, huenda akashawishika kurudi England kwenda kumalizia kiporo chake cha kuwa kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu England.
Kane anataka kuvunja rekodi ya Alan Shearer ya kufunga mabao 260 kwenye Ligi Kuu England. Kane alifunga mabao 213 katika mechi 320 alizochezea Tottenham kabla ya kuhamia Bayern kwa ada ya Pauni 100 milioni mwaka 2023. Kwa maana hiyo, bado mabao 47 kumfikia Shearer, ambaye aliweka rekodi hiyo kwa kucheza mechi 441 alizocheza kwenye kikosi cha Blackburn Rovers na Newcastle United.
Licha ya namba zake kuwa tamu Bayern, akiwa amefunga mabao 57 katika mechi 58 za Bundesliga na mabao 73 katika mechi 78 za michuano yote, Kane haonekani kama mchezaji muhimu kwenye timu hiyo, akikosolewa kwa sababu hafungi mabao ya nje ya 18 na amekuwa hatambi kwenye mechi kubwa.
Na kwenye hilo, Bayern ilitangaza wazi kwamba Kane anaweza kupatikana sokoni kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kama itawekwa mezani Pauni 67 milioni.
Na kama Kane atarudi kwenye Ligi Kuu England, ambapo Julai mwaka huu atafikisha umri wa miaka 32, kuna timu nne zinahitaji huduma yake bila shaka.
Spurs inaweza kuwa chaguo lake la kwanza, kurudi hapo kwenye kuendelea na rekodi yake ya kufunga mabao, ambako akifukuzia pia rekodi za kinara wa muda wote wa mabao kwenye timu hiyo, Jimmy Greaves, aliyefunga mara 280 katika mechi 435.
Arsenal ni miamba mingine, ambayo inaweza kuchagua kumrudisha mchezaji huyo aliyewahi kuwa kwenye timu yao 2001. Arsenal inahitaji kuwa na mtu mwenye uhakika wa kufunga mabao ili kutimiza lengo lao la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England na kama kuna mchezaji wa aina hiyo wanayemsaka, Kane anaweza kuwa suluhisho.
Chelsea ni miamba mingine ambayo inaweza kumrudisha Kane kwenye Ligi Kuu England, ambapo straika huyo anaweza kwenda kuwa suluhu la mabao kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge.
Manchester United mara nyingi imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili Kane huko nyuma na pengine sasa hivi inaweza kurudi haraka kunasa saini ya mchezaji huyo, hasa katika nyakati hizi ambazo imekuwa ikihitaji straika wa kuwafungia mabao baada ya Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee kushindwa kufanya mambo ya maana Old Trafford.