Haaland aibeba Norway ikiiduwaza Iraq Kombe la Dunia
Muktasari:
- Imewachukia dakika 29 tu Norway kuandika bao la kwanza kwenye mchezo huo, Haaland akifunga kwa mguu wa kushoto akimalizia krosi ya beki wake wa kushoto David Wolfe.
Norway imeanza vizuri Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuichapa Iraq kwa mabao 4-1 muuwaji akiwa mshambuliaji Erling Halaland.
Imewachukia dakika 29 tu Norway kuandika bao la kwanza kwenye mchezo huo, Haaland akifunga kwa mguu wa kushoto akimalizia krosi ya beki wake wa kushoto David Wolfe.
Hata hivyo Iraq ikafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 39, mfungaji akiwa Aymen Hussein, akimalizia kwa kichwa kizuri krosi ya Amir Al Ammari.
Bao hilo la Hussein linakuwa la 34 kwa Taifa lake akiwa mmoja wa washambuliaji waliofunga mabao mengi.
Haaland akairudisha Norway tena kuongoza, akifunga bao la pili akinufaika na makosa ya beki wa Iraq na kipa wake Jalal Hassan walioshindwa kuokoa mpira baada ya kupigiana pasi fupi na mshambuliaji huyo kufunga.
Mpaka mapumziko Norway ikatoka na uongozi wa mabao 2-1 huku pia timu hizo zikishambuliana kwa zamu.
Alikuwa Leo Ostigard akiimaliza Iraq baada ya kupiga bao la tatu kwa kichwa dakika ya 76 akimalizia mpira wa Kona ya Martin Odegaard.
Wakati mchezo huo ukielekea mwisho Hussein akaipa bao la nne Norway akijifunga wakati akipambana kuokoa na kufanya mchezo huo kumalizika kwa ushindi wa Norway wa mabao 4-1.
Mabao hayo mawili yanamfanya Haaland kufikisha mabao 52 kwenye timu ya Taifa akiendeleza rekodi yake bora ya kufunga.
Norway imeendelea kuonyesha ubora kwenye mechi za kwanza katika fainali za Kombe la Dunia ambapo haijawahi kupoteza mchezo wa kwanza.