Gwiji Sauzi awashukia Kaze, Youssef, ataka mabadiliko Kaizer Chiefs
Muktasari:
Ngubane anaamini kuwa, Chiefs hawajaonyesha maendeleo bora chini ya uongozi wa makocha Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze, akitaja ukosefu wa mbinu bora za uchezaji ni kama tatizo kuu ndani ya timu hiyo.
KUTOKANA na kile kinachoendelea ndani ya Kaizer Chiefs, gwiji wa soka wa Afrika Kusini, Mlungisi Ngubane anaamini huu ni wakati muafaka klabu hiyo kufanya mabadiliko katika benchi la ufundi ili kujiandaa vyema na msimu ujao.
Ngubane anaamini kuwa, Chiefs hawajaonyesha maendeleo bora chini ya uongozi wa makocha Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze, akitaja ukosefu wa mbinu bora za uchezaji ni kama tatizo kuu ndani ya timu hiyo.
Pia amehoji sababu za kutompa nafasi zaidi kinda Mfundo Vilakazi, akirejea kiwango chake bora katika Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 20, ambako alionyesha uwezo mkubwa akiwa na mpira miguuni.
“Ukubwa wa mwili wa mchezaji haupaswi kuwa tatizo; Vilakazi ana ukubwa unaolingana na wachezaji maarufu kama Lionel Messi. Hata hivyo, Kaze na Youssef wanaonekana kukosa imani kwa vipaji hivi vya vijana,” amesema Ngubane maarufu kwa jina la utani Professor.
Mchezaji huyo wa zamani wa Durban Bush Bucks, ameongeza kuwa licha ya Mduduzi Shabalala kuonyesha kutokuwa na mwendelezo mzuri, bado anaikumbuka michango yake akiwa kwenye DStv Diski Challenge wakati Chiefs wanapocheza bila mwelekeo.
Ngubane amesisitiza kuwa mpangilio wa sasa wa makocha ndani ya klabu hiyo hauridhishi, akidai makocha hao wawili awali waliwekwa kama wakalimani wa kocha aliyekuwa hana ufasaha wa Kiingereza, badala ya kuwa sehemu ya benchi la ufundi lenye mamlaka kamili.
Amebainisha kuwa, mara nyingi wawili hao huonekana kusimama pembeni wakiwa hawatoi maelekezo madhubuti, jambo linaloashiria ukosefu wa uongozi wa kimkakati. Kwa mtazamo wake, kocha anapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja kutoka benchi wakati wa mechi ili kuipa timu mwelekeo.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu kadhaa za PSL, amependekeza klabu hiyo iwatafakari Pitso Mosimane au Rulani Mokwena, akisema wana ukomavu na uelewa wa kiufundi wa kuiongoza Chiefs.
Amesema hasa Mokwena ana uwezo wa kuisimamia timu bila kuwachosha wachezaji kwa maelekezo mengi na tafiti zisizo za lazima, jambo ambalo mara nyingi halipendwi na wanasoka.
Mwisho, Ngubane ameishauri menejimenti ya Kaizer Chiefs kuwakabidhi Vela Khumalo na Dillon Sheppard jukumu la kusimamia mfumo wa vijana hadi pale kocha mpya atakapopatikana, akisisitiza kuwa wawili hao wana uelewa mzuri wa vipaji vya chipukizi vya klabu hiyo.
Ikumbukwe kuwa, Youssef na Kaze kwa sasa wanaongoza benchi la ufundi la timu hiyo tangu kuondoka kwa Nasreddine Nabi Septemba 2025 ambapo makocha hao wawili walikuwa wasaidizi wake.
Kaizer Chiefs kwa sasa ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL) baada ya kucheza mechi 16 ikikusanya pointi 30. Imeachwa pointi nane na vinara Mamelodi Sundowns yenye 38 ikishuka dimbani mara 17.
Timu hiyo imemaliza nafasi ya tatu katika Kundi D la Kombe la Shirikisho msimu huu na kushindwa kufuzu robo fainali ikimaliza na pointi 10 sawa na Al Masry iliyoshika nafsi ya pili zikitofautiana mabao.
Pia Kaizer imeondoshwa katika michuano ya Nedbank Cup hatua ya 32 Bora ilipofungwa 2-1 na Stellenbosch, kumbuka ndiyo ilikuwa bingwa mtetezi.