Guler na Alonso wanaendelea kuwasiliana, uhamisho mgumu
Muktasari:
- Alonso aliifundisha Real Madrid kwa siku 233 kabla ya kutimuliwa kutokana na matatizo kibao yaliyoanza wakati wa utawala wake yaliyohusisha masuala ya uhusiano wake na wachezaji pamoja na mashabiki kwa upande mwingine.
MADRID, HISPANIA: HATA kabla hajaanza rasmi kazi, kocha mpya wa Chelsea Xabi Alonso anaweza kujikuta matatani iwapo Real Madrid aliyoifundishwa kwa miezi saba na nusu itaamua kumchukulia hatua mahakamani, baada ya kufichuka ujumbe wake wa mfupi wa simu ambao amekuwa akimtumia nyota wa mabingwa hao wa zamani wa Hispania, Arda Guler.
Alonso aliifundisha Real Madrid kwa siku 233 kabla ya kutimuliwa kutokana na matatizo kibao yaliyoanza wakati wa utawala wake yaliyohusisha masuala ya uhusiano wake na wachezaji pamoja na mashabiki kwa upande mwingine.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wachezaji walimpenda kufurahia kipindi cha ukocha wa nyota huyo wa zamani wa kikosi hicho na Liverpool aliyeng'ara pia kwa kubeba ubingwa wa Bundesliga akiwa na Bayer Leverkusen 2022/23 na miongoni mwao akiwamo Guler wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara.
Kocha huyo ambaye anatarajiwa kuanza kuinoa Chelsea kwa mkataba wa miaka minne kuanzia Julai Mosi, anaaminika kuwa tayari anashiriki kwa karibu katika mipango ya awali ya usajili wa wachezaji na amekuwa akiwashawishi mastaa aliowahi kupiga nao kazi katika timu alizoifundisha na hapo ndipo Real Madrid inafikiria kuanzisha uchunguzi ili imchukulie hatua iwapo itabainika anamshawishi Guler kuondoka ilhali ana mkataba wa miaka mitatu.
Kipindi kifupi lakini chenye mafanikio cha Alonso akiwa Madrid kilimsaidia kujenga uhusiano mzuri wa kikazi na Guler, ambapo awali mchezaji huyo wa kimataifa wa Uturuki alikuwa akipata nafasi chache za kucheza chini ya makocha waliomtangulia Alonso, lakini mambo yalibadilika kwa kiasi kikubwa baada ya kuwasili.
Chini ya uongozi wake, Guler alipewa imani zaidi na majukumu makubwa uwanjani na mabadiliko hayo yalimsaidia kuwa mchezaji muhimu zaidi kikosini na kuimarisha uhusiano wake na kocha huyo Mhispania, na hata baada ya Alonso kuondoka inaonekana kuwa uhusiano huo umeendelea kupitia mawasiliano yao ya faragha.
Viongozi wa Chelsea wanafahamu kwamba mahusiano binafsi ya Alonso yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika uamuzi wa usajili na taarifa zinaeleza kuwa tayari ameshawasilisha majina ya wachezaji anaoamini wanaweza kuboresha kikosi, huku Güler akiwa juu ya orodha hiyo.
Wazo la kuungana tena Stamford Bridge linadaiwa kumvutia Alonso, hasa kutokana na uwezo wa kiufundi wa kiungo huyo na nafasi yake kubwa ya kuendelea kuimarika siku zijazo, lakini Real Madrid inaamini kwamba bado ni mchezaji muhimu kwao na hawataki ashawishiwe bila kwanza kupata idhini kutoka kwao.
Guler akimzungumzia Alonso, alisema kwa hisia kuwa walikuwa na uhusiano wa karibu uliojengwa juu ya kuaminiana na ni miongoni mwa makocha anaoamini kwamba waliipenda kazi yake Madrid.
“Kwa kweli tulikuwa na uhusiano mzuri sana. Nilihisi kana kwamba alikuwa amenikabidhi funguo za timu. Hicho ndicho hasa nilichokuwa nikikitafuta. Sasa amesaini Chelsea. Natumaini kila kitu kitamwendea vizuri. Bila shaka bado tunatumiana ujumbe,” alisema mchezaji huyo.
Hata hivyo, uhamisho wowote wa kwenda Chelsea hautakuwa rahisi, kwani hata kama Reak Madrid itaamua kupotezea kumshtaki Alonso, basi Chelsea italazimika kulipa Euro 100 milioni ili kumnunua.