Guehi kuleta shida Januari 2026
Muktasari:
- Guehi, 25, alikaribia kabisa kujiunga na Liverpool kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, lakini dili hilo lilikwama dakika za mwisho.
BIRMINGHAM, ENGLAND: BEKI wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi huenda akasababisha vita kali kwenye dirisha lijalo la usajili wa Januari baada ya vigogo kibao huko Ulaya kuhitaji huduma yake.
Guehi, 25, alikaribia kabisa kujiunga na Liverpool kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, lakini dili hilo lilikwama dakika za mwisho.
Crystal Palace ilikubali ada ya Pauni 35 milioni ya kumuuza beki huyo ambaye amebakiza muda usiozidi mwaka mmoja katika mkataba wake huko Selhurst Park. Dili la kutua Anfield lilitarajia kukamilika mapema Jumatatu na Guehi alishaandaa kabisa video ya kuaga Palace.
Lakini, Palace ilishindwa kupata beki mwingine wa kuja kuchukua nafasi yake jambo lililomfanya kocha Oliver Glasner kutishia kubwaga manyanga endapo kama nahodha wake huyo angepigwa bei na ndio maana, Palace ikasitisha kumuuza dakika za mwisho. Glasner sasa atabaki Palace baada ya Guehi kubaki na mara zote amekuwa profesheno.
Ripoti zinafichua kwamba Liverpool imepanga kurudi kwenye dili la kumtaka beki huyo wakati wa dirisha la Januari, ambapo Guehi itakapofika Januari 1 mwakani, atakuwa huru kusaini mkataba wa awali na klabu za nje ya England.
Kutokana na hilo, miamba miwili ya Hispania, Barcelona na Real Madrid imeshaanza mchakato wa kutaka kwenda kunasa saini yake. Liverpool yenyewe inamtaka Guehi kutokana na beki wake wa kati, Ibrahima Konate kuhusishwa na mpango wa kujiunga na Real Madrid, huku mkataba wake ukitarajia kufika ukingoni Juni mwakani.
Guehi ambaye alikuwa tayari kuachana na Palace baada ya kucheza hapo kwa misimu minne alisema: “Mimi ni kijana wa London kusini; nimekulilia huko na nimekuwa nahodha wa klabu hii tangu nikiwa na umri mdogo. Imekuwa klabu bora kwangu na familia yangu. Ni furaha kubwa kuwa kwenye klabu hii.”