Guardiola: Hata tukishinda Arsenal, ubingwa bado mbali
Muktasari:
- Guardiola alisema wazi kuwa kushindwa katika mchezo wa leo, Jumapili kutakuwa na madhara makubwa katika matumaini yao ya ubingwa lakini hata wakishinda bado safari haitakuwa rahisi.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, ameeleza kuwa hata kama timu yake itashinda mechi muhimu dhidi ya Arsenal leo haitakuwa timu inayopaswa kupigiwa hesabu zaidi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Guardiola alisema wazi kuwa kushindwa katika mchezo wa leo, Jumapili kutakuwa na madhara makubwa katika matumaini yao ya ubingwa lakini hata wakishinda bado safari haitakuwa rahisi.
“Ukishindwa, basi ndio mwisho wa matumaini,” alisema Guardiola.
“Lakini bado kuna michezo sita au saba, hivyo kila kitu bado kinawezekana.”
Aliongeza kuwa ratiba ya Manchester City ni ngumu sana, akitaja mechi dhidi ya Everton ugenini, Bournemouth ugenini, Aston Villa nyumbani, pamoja na Crystal Palace na Brentford.
Guardiola alisisitiza kuwa ligi bado haijaamuliwa na kila kitu kinaweza kubadilika kwa haraka.
“Hatujui kitakachotokea. Labda wiki chache zilizopita hatukuwa na matumaini makubwa lakini sasa bado tupo kwenye mbio,” alisema.
Kocha huyo pia alisisitiza umuhimu wa timu yake kucheza kwa kiwango bora kabisa ili kupata matokeo dhidi ya Arsenal.
“Ukicheza kama tulivyocheza kipindi cha pili kwenye fainali ya Carabao Cup kwa dakika 95, basi tuna nafasi kubwa ya kushinda,” alisema.
Hata hivyo alionya kuwa soka haliwezi kutabiriwa kwa urahisi.
“Sio kila kitu kinategemea mpango. Lazima tufanye kazi kwa kiwango cha juu kabisa,” aliongeza.
Guardiola pia alitambua nguvu ya Arsenal msimu huu, akisema wana faida ya kujiamini kutokana shauku waliyonayo muda mrefu ya kuhitaji ubingwa huo.