Guardiola amweka binti yake benchi

Muktasari:
- Man City ilianza vyema michuano hiyo baada ya kuichapa timu hiyo ya Morocco, Wydad Casablanca mabao 2-0. Ushindi huo ulimfanya Guardiola, 54, atulie bila ya wasiwasi wowote uwanjani Lincoln Financial Field huko Philadelphia, Marekani.
PHILADELPHIA, MAREKANI: KOCHA, Pep Guardiola ameamua kumwanika binti yake, Valentina kwa mashabiki wa soka duniani baada ya kumkaribisha kwenye benchi la ufundi wakati Manchester City ilipokuwa katika majukumu ya kumenyana na Wydad kwenye mechi yao ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
Man City ilianza vyema michuano hiyo baada ya kuichapa timu hiyo ya Morocco, Wydad Casablanca mabao 2-0. Ushindi huo ulimfanya Guardiola, 54, atulie bila ya wasiwasi wowote uwanjani Lincoln Financial Field huko Philadelphia, Marekani.
Kocha Guardiola alikuwa ametulizana wakati wachezaji wake wakifanya jambo uwanjani. Aliungana na binti yake, mrembo Valentina, 17, na kupiga stori kwenye benchi la ufundi.
Jambo hilo liliwafanya mashabiki kutania kwamba huenda bosi mpya ametua kwenye benchi la ufundi.
Valentina ni mtoto wa mwisho wa Guardiola kwenye orodha ya watoto wake watatu aliozaa na mkewe, mrembo Cristina Serra. Binti yake mkubwa, Maria, 24, ni mwanamitindo na mhamasishaji wa mtandaoni mwenye wafuasi zaidi ya 100,000 huko Instagram.
Mwanaye wa kiume, Marius, 22, ni mfanyabiashara mwenye biashara nyingi, lakini ameamua kufanya mambo yake kimyakimya. Ripoti za Februari mwaka huu ni kwamba Guardiola aliingia kwenye mazungumzo ya kutalikiana na mkewe Cristina. Wanandoa hao wamekuwa pamoja kwa miaka 30.
Familia ya Pep imekuwa ikijitokeza hadharani mara chache sana na mara nyingi huwa ni katika kushangilia ubingwa, ambapo ilionekana uwanjani wakati wa kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu England miaka miwili iliyopita.
Lakini, sasa binti yake Valentina alikuwa kwenye benchi la ufundi wakati Man City ikifunga mabao yake kupitia kwa Phil Foden na Jeremy Doku.
Mechi ijayo ya Man City itapigwa Jumatatu ijayo dhidi ya Al-Ain kabla ya kumalizana na Juventus huku ikiwa haifahamiki kama binti huyo ataendelea kuwapo kwenye benchi.