Guadiola: Kesi ya Man City isikilizwe

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola anataka kesi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City juu ya matumizi mabaya ya pesa isikilizwe sasa — ili wasafishe jina lao. Mabosi wa Ligi Kuu England waliishtaki Man City kwa tuhuma za kutenda makosa 115 ya matumizi ya hovyo ya pesa kwenye usajili waliyofanya kati ya mwaka 2009 hadi 2018.
Wengi wanadhani shutuma hizo zinaweka ukakasi kwenye mafanikio makubwa ya klabu hiyo, ambapo kwa msimu huu inafukuzia mataji matatu, baada ya kubeba gtaji la Ligi Kuu England na imeshafika fainali ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini, Guardiola anataka sakata hilo limelizwe haraka ili kuthibitisha kwamba Man City haina kitu kibaya ilifanya tangu walipokuwa chini ya umiliki wa matajiri wa Abu Dhabi mwaka 2008.
Kocha Guardiola alisema: “Kitu ambacho ningependa kama Ligi Kuu England na majaji wanaweza kufanya jambo hilo kwa haraka zaidi — hivyo kama kuna kitu tumekosea basi kifahamike. Kama tupo kama tunavyoamini tupo — klabu kwamba kwa miaka mingi imekuwa ikifanya vitu kwa usahihi, basi watu wataanza kutuzungumzia vibaya.
“Tungependa ifanywe hata kesho — ikiwa leo ni vizuri zaidi. Tungependa iwe hivyo. Tunaamini hawapo bize sana na majaji watakutana na pande mbili kuona kipi ni bora. Mwisho wa yote, najua haki kabisa tulichokishinda ni cha uwanjani na hatuna shaka yoyote.”
Man City haijapoteza mechi yoyote tangu washtakiwe mwanzoni mwa Februari na wikiendi iliyopita ilishinda taji lake la tatu mfululizo la Ligi Kuu England. Na sasa wamebakiza ushindi kwenye mechi mbili tu kukamilisha mataji matatu ya msimu huu, wakibaliana na Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA na Inter Milan kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, Guardiola alisema: “Tumekubali kwamba lipo. Kama imetokea, imetokea. Ilikuwa hivyo na Uefa na sasa ni Ligi Kuu England. Haya twende kazi, ndani ya saa 24, kaeni chini na wanasheria waweke vitu hadharani.
“Isisubiriwe miaka miwili. Tumalizane haraka iwezekanavyo kwa manufaa ya kila mtu. Tunataka kulinda heshima yetu na kama wanatia shaka, sawa, tumalizane nalo haraka, tafadhali.”
Guardiola alisaini mkataba mpya wa miaka miwili Novemba mwaka jana wa kuendelea kubaki kwenye klabu hiyo ya Man City, hivyo atakuwapo Etihad hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2025. Alisema hataondoka kama keshi hizo zitakuwa hazijamalizwa  — lakini kumekuwa na maelezo kwamba huenda akaachana na miamba hiyo endapo itanyakua mataji matatu msimu huu.
Fainali yao ya kwanza itakayokuwa ya Kombe la FA itapigwa Juni 3 huko Wembley, wakati fainali ya pili watakayocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya itakuwa wiki moja baadaye huko Istanbul, Uturuki.
Kocha, Guardiola, mwenye umri wa miaka 52 alisema: “Nitaendelea kuwapo msimu ujao wakati tukiwa na makosa 110 dhidi yetu. Msijali. Lakini, sifahamu itakuwaje kwenye ishu ya kushinda au kupoteza nafasi hizi mbili tulizopata. Nina mkataba na niliposaini, niliweka wazi nataka kuiheshimu klabu.