Grealish kujinoa kivyake Etihad
Muktasari:
- Grealish, 29, anajiandaa kuachana na maisha ya Etihad kwenye dirisha hili baada ya kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza msimu uliopita.
MANCHESTER, ENGLAND: JACK Grealish ameripotiwa kukubali kufanya mazoezi kivyake wakati huu akijiandaa na mpango wa kuachana na Manchester City kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Grealish, 29, anajiandaa kuachana na maisha ya Etihad kwenye dirisha hili baada ya kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza msimu uliopita.
Winga huyo ameshindwa kumshawishi kocha Pep Guardiola ili kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha miamba hiyo baada ya kuanzishwa kwenye mechi saba tu za Ligi Kuu England msimu uliopita.
Kocha Guardiola alimweka kando Grealish kwenye kikosi chake cha Man City kilichokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
Kwa mujibu wa Telegraph, Grealish sasa amekubali kurudi Man City kufanya mazoezi kivyake wakati huu akisubiria hatima ya maisha yake ya soka.
Hadi wakati huu, Grealish anafanya mazoezi kwa usimamizi wa kocha wake binafsi ikiwa ni kujiweka sawa ili kusubiri ofa ya kubadilisha timu.
Mkali huyo wa zamani wa Aston Villa atarejea mazoezini Man City wikiendi hii, wakati kikosi kingine cha mastaa wa timu hiyo, kitaingia mazoezini kwa ajili ya pre-season, Julai 28. Grealish inaelezwa ameambiwa anaweza kuondoka, lakini bado hajapata dili.
Hata hivyo, mshahara mkubwa wa staa huyo, ambaye aliigharimu Man City Pauni 100 milioni wakati iliponasa saini yake mwaka 2021, unaweka ugumu wa dili lake kutokea akisakwa na timu kibao za EPL zikiwamo West Ham na Everton.