FIFA yaja na mpango huu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mfumo huo mpya unaripotiwa kuwa utazisaidia timu nne za juu kwenye viwango vya dunia vya FIFA kwa kuwatenganisha na hazitokutana labda zifike nusu fainali.
NEW YORK, MAREKANI: SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limepanga kutumia mfumo mpya wa upangaji hatua ya makundi na droo kwa ujumla katika michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza mwakani huko Marekani, Mexico na Canada msimu ujao.
Mfumo huo mpya unaripotiwa kuwa utazisaidia timu nne za juu kwenye viwango vya dunia vya FIFA kwa kuwatenganisha na hazitokutana labda zifike nusu fainali.
Hiyo ina maana kwamba Hispania, England, Ufaransa na Argentina, ambazo ndio zinaongoza katika orodha hiyo hazitoweza kukutana hadi nusu fainali na fainali.
England italazimika kukutana na Hispania au Argentina kwenye nusu fainali ili kufuzu fainali, na wanaweza kukutana na Ureno, Ujerumani, Brazil au Uholanzi robo fainali.
Muundo kamili wa makundi 12 utatolewa kwenye droo ya fainali itakayofanyika Washington DC, Marekani Desemba 5, baada ya FIFA kulazimika kubadilisha mfumo ambao sasa unaruhusu England kukutana na Scotland au Norway ya Erling Haaland ambazo hazikufuzu moja kwa moja.
Pendekezo la awali la FIFA lilitaka timu 12 za Ulaya zilizofuzu moja kwa moja zigawanywe kila moja kwenye makundi 12.
England iko kwenye kapu linalojumuisha mataifa tisa bora duniani kwa sasa na wenyeji watatu Canada, Mexico na Marekani ambao hawatokutana katika hatua ya makundi.
Timu 42 zilizobaki zitapangwa kwa mujibu wa viwango vya FIFA.