Fenerbahce yamtema Jose Mourinho
Muktasari:
- Klabu hiyo yenye maskani yake jijini Istanbul imetoa taarifa mapema leo Ijumaa inayothibitisha kuondoka kwa kocha huyo wa Ureno, aliyekuwa amepewa jukumu la kuliongoza benchi la ufundi kwa matarajio makubwa mwaka 2024.
Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki imemfuta kazi kocha mkuu Jose Mourinho.
Klabu hiyo yenye maskani yake jijini Istanbul imetoa taarifa mapema leo Ijumaa inayothibitisha kuondoka kwa kocha huyo wa Ureno, aliyekuwa amepewa jukumu la kuliongoza benchi la ufundi kwa matarajio makubwa mwaka 2024.
Jose Mourinho (62) ameondoka Fenerbahce siku moja tu baada ya kikosi cha timu hiyo kupoteza mchezo wa kufuzu Ligi ya Mabingwa dhidi ya Benfica.
Meneja huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United, na Tottenham alijiunga na Fenerbahce msimu wa joto wa 2024, miezi sita baada ya kutimuliwa na AS Roma ya Italia.
Aliiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita, lakini alishindwa kupata taji lolote, akiondoshwa Kombe la Uturuki hatua ya robo fainali na Europa League ikiwa 16 Bora.
Fenerbahce ilifungwa 1-0 na Benfica katika mchezo wa mkondo wa pili wa mchujo wa kuwania kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa, kufuatia sare ya 0-0 Istanbul wiki iliyopita.