Fenerbahce: Rashford? Hapana, hatumtaki
Muktasari:
- Rashford anatarajia kuachana na maisha ya Old Trafford kwenye dirisha hili la Januari, baada ya kuwekwa kando na kocha Ruben Amorim.
ISTANBUL, UTURUKI: BOSI wa Fenerbahce inayonolewa na Jose Mourinho, Acun Ilicali amesema tena kwa msisitizo hawana mpango wa kumsajili staa wa Manchester United, Marcus Rashford.
Rashford anatarajia kuachana na maisha ya Old Trafford kwenye dirisha hili la Januari, baada ya kuwekwa kando na kocha Ruben Amorim.
Barcelona ipo mstari wa mbele kumsajili kwa mkopo, lakini tatizo la kiuchumi linaonekana kuwa ni shida.
Timu kadhaa zimekuwa zikihusishwa na Rashford, ikiwamo miamba ya Uturuki - Fenerbahce ambayo kwa sasa inanolewa na aliyekuwa kocha wa Man United, Chelsea, Real Madrid, Tottenham Hotspur, AS Roma, Inter Milan na FC Porto, Mourinho.
Lakini, makamu wa rais wa Fenerbahce, Ilicali, alifichua kwamba walipewa ofa ya kumchukua mchezaji huyo, ila hawana mpango naye. “Ukweli kumekuwa na taarifa tunavutiwa na mchezaji huyo,” alisema.
“Nadhani Rashford ni mchezaji mahiri, nampenda. Lakini, mwisho wa yote unapokuwa na mchezaji kwenye timu yako anayecheza nafasi kama yake inakuwa haina maana kuwa na mwingine kwenye eneo hilo. Ninachoweza kusema ni kwamba aina hii ya wachezaji wanataka kucheza muda wote, hivyo akija mmoja wa wachezaji wetu hatacheza. Hilo suala lilipoletwa mbele yetu kwa bahati mbaya tulisema hakuna mpango huo usajili.
“Hatuna kinachotuvutia kwake. Ni kweli uvumi unasambaa kwa kasi sana. Ninachosema kisichokuwa na shaka hatuvutiwi naye, lakini ni mchezaji mzuri.”
Rashford hajaichezea Man United mechi 11.