Febregas aitega Chelsea akiitaka EPL
Muktasari:
- Fabregas ambaye amekuwa akihusishwa na nafasi ya ukocha Stamford Bridge baada ya kufutwa kazi kwa Liam Rosenior, amesema hana haraka ya kuondoka Como licha ya mafanikio anayopata.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Como, Cesc Fabregas ameweka wazi kuwa anatamani siku moja kufundisha katika Ligi Kuu ya England lakini ameonya kuwa hatakubali kazi ambayo hatakuwa na sauti kwenye maamuzi kitu ambacho kinaweza kuipa wakati mgumu Chelsea inayovutiwa naye.
Fabregas ambaye amekuwa akihusishwa na nafasi ya ukocha Stamford Bridge baada ya kufutwa kazi kwa Liam Rosenior, amesema hana haraka ya kuondoka Como licha ya mafanikio anayopata.
Kocha huyo kijana ameweka wazi kuwa anahitaji mazingira yenye imani na uhuru wa kufanya maamuzi, hususani katika usajili wa wachezaji jambo ambalo linaweza kuwa changamoto kwa mfumo wa Chelsea unaotumia wakurugenzi wa michezo.
“Nataka kuwa na mamlaka ya maamuzi ya soka. Usajili lazima uwe kitu ninachoamini,” alisema Fabregas akisisitiza kuwa kwa sasa anafurahia kazi yake Como ambako ana uhuru mkubwa wa kuendesha timu.
Aliongeza kuwa soka hubadilika haraka, hivyo hana presha ya kukimbilia katika Ligi Kuu ya England kwa sasa.
Akiwa mchezaji, Fabregas aliwahi kung’ara akiwa na Chelsea kati ya mwaka 2014 hadi 2019, akishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England.
Como imekuwa moja ya timu zinazovutia nchini Italia chini ya kocha huyo baada ya kupanda daraja mwaka 2024 na sasa inapambana kufuzu michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza.
Ikiwa zimesalia mechi tatu kumaliza msimu kwa msimu huu wa Serie A, timu hiyo ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 62 nyuma ya Juventus iliyopo nafasi ya nne kwa tofauti ya pointi tatu.