Fainali UEFA CL: Mashabiki kufungua mifuko, Sh10 milioni kuhusika
Muktasari:
Arsenal walitinga fainali baada ya kuichapa Atletico Madrid jumla ya mabao 2-1, huku PSG ikitinga kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuichapa Bayern Munich jumla ya mabao 6-5.
BUDAPEST, HUNGURY: UNATAKA kuziona Arsenal na Paris Saint Germain? Utaweza ila tu uhakikishe mfuko wako haukosi chini ya Sh10 milioni. Hapo ni kuanzia jijini London na kama unaanzia Tanzania au Afrika kwa jumla, ujipange zaidi.
Ndiyo, gharama za kuiona fainali hiyo inayotarajiwa kupigwa Mei 30, si mchezo na inaelezwa kwa kadirio la haraka shabiki atakayetoka London hadi Budabest, Hungary kunakofanyika fainali hiyo awe na kiasi cha Pauni 3000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh10 milioni.
Arsenal walitinga fainali baada ya kuichapa Atletico Madrid jumla ya mabao 2-1, huku PSG ikitinga kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuichapa Bayern Munich jumla ya mabao 6-5.
Arsenal inasaka taji lake la kwanza la Uefa, huku PSG ikilitetea baada ya msimuuliopita kubeba ikiwa ni mara yao ya kwanza na kuifanya mechi hiyo kuwa ya mkwanja kutokana na gharama zake kupanda.
Inaelezwa, mashabiki wa timu hizo watakaotaka kwenda huko, lazima wawe na bajeti ya kutosha kwani gharama za tiketi na hoteli hazishikiki tangu kuanza kwa mwezi huu na wanahangaika kukata tiketi za ndege na kulipia hoteli baada ya timu zao kutinga fainali.
Mara tu baada ya Arsenal kutinga fainali, bei ya tiketi za ndege kwenda na kurudi Budapest kutoka London zimepanda kwa kasi hadi kufikia Pauni 1,200 kwa usiku mmoja kutoka Pauni 700 hadi 800 hapo awali.
Tiketi za moja kwa moja za bei nafuu zaidi zilizopo sasa zimevuka Pauni 900, huku kiasi hicho kikitarajiwa kuongezeka zaidi katika siku zijazo.
Mashabiki wasiopenda kulipa gharama hizo kubwa za ndege wanaweza kutumia basi kwenda na kurudi Budapest litakalotumia saa 42 kwa gharama ya Pauni 269.
Hata hivyo, kwa mashabiki wa PSG bei za ndege zinaonekana kuwa rahisi zaidi ikizingatia hakuna umbali kutoka Ufaransa hadi Hungury.
Tiketi za kutoka Paris hadi Budapest za bei ya juu zaidi kwa sasa zinafikia Euro 700 kwenda na kurudi ambayo imepanda ikilinganishwa na gharama ya awali ya Euro 300 hadi 400.
Hoteli nazo zimekuwa tatizo kubwa na hadi kufikia jana tovuti maarufu ya Booking.com ilikuwa inaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya vyumba vilivyokuwa vinapatikana tayari vimechukuliwa.
Vyumba vya bei nafuu zaidi vilivyosalia jijini humo sasa vinapatikana katika hosteli ambayo kwa usiku mmoja vinagharimu Pauni 250.
Mbali ya shida ya hoteli na usafiri, tiketi za fainali zenyewe zinatarajiwa kuwa za gharama kubwa zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tiketi za bei ya chini kabisa ni Pauni 60, huku tiketi za daraja la tatu zikiuzwa kwa Pauni Pauni 155 na la pili zikiuzwa kwa Pauni 560 mtawalia na za daraja la kwanza ni Pauni 819.