Esperance walia na ubora wakitupwa nje Kombe la Dunia

Muktasari:
- Katika mchezo huo, Chelsea imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 ambao umeifanya imalize katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D la mashindano hayo na kutinga hatua ya 16.
Esperance imekiri kwamba ubora wa Chelsea dhidi yao umeamua kwa kiasi kikubwa matokeo ya mchezo baina yao katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Klabu iliyochezwa Alfajiri ya kuamkia leo Juni 25, 2025 katika Uwanja wa Financial Field, Philadelphia.
Katika mchezo huo, Chelsea imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 ambao umeifanya imalize katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D la mashindano hayo na kutinga hatua ya 16.
Kwa upande mwingine matokeo hayo yamemaanisha kwamba Esperance imeaga rasmi mashindano na kocha wao Maher Kanzar anaamini kwamba wapinzani wao walikuwa bora katika namna walivyozifanyia kazi nyakati muhimu ndani ya uwanja.
“Mpira wa Miguu unachezwa kwa dakika 90 ukijumuisha muda unaopotezwa. Tulizicheza dakika 45 lakini tukasahau kuhusu muda uliopotezwa. Tulipoteza umakini wakati wa dakika zilizopotezwa kipindi cha kwanza wakati wa friikiki.
“Kabla ya hapo, tulikuwa vizuri katika mashambulizi ya kushtukiza na kutengeneza hatari karibu na goli lao. Ndio walikuwa na nafasi kwa sababu ya utofauti katika ubora lakini tulikuwa vizuri kimbinu.
“Baada ya goli la kwanza, la pili likaja kwa haraka pia kwa sababu ya kupoteza umakini. Kipindi cha kwanza kiliamua mchezo. Hakuna cha muhimu kilichotokea kipindi cha pili,” amesema Kanzari.
Esperance sasa imeungana na wawakilishi wengine wawili wa Afrika, Wydad Casablanca na Al Ahly kuaga mashindano hayo.
Kwa sasa matumaini pekee ya Afrika yamebaki kwa Mamelodi Sundowns ambayo leo saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki itakabiliana na Fluminense ya Brazil.
Sundowns inahitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi hiyo ili iweze kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.