Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

England yaanza na ushindi Kombe la Dunia, mvua ya mabao yatawala

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo ilishuhudia England ikipata bao la utangulizi dakika ya 12, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Harry Kane kwa mkwaju wa penalti ya kurudia baada ya kwanza aliyopiga kukosa.

TEXAS, MAREKANI: TIMU ya taifa ya England imeanza vyema Michuano ya Kombe la Dunia, baada ya kuifunga Croatia mabao 4-2, katika mechi kali na ya kuvutia ya kundi L iliyopigwa kwenye Uwanja wa Dallas huko Arlington, Texas, Marekani

Katika mechi hiyo ilishuhudia England ikipata bao la utangulizi dakika ya 12, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Harry Kane kwa mkwaju wa penalti ya kurudia baada ya kwanza aliyopiga kukosa.

Nyota huyo alirudia penalti hiyo na kufunga baada ya kipa wa Croatia, Dominik Livakovic kutoka mbele ya mstari mapema kabla ya Kane kupiga penalti hiyo iliyotokana na madhambi aliyofanyiwa, Noni Madueke akiwa eneo la hatari na kiungo, Luka Modric.

Bao hilo ndilo lililoiamsha Croatia na kusawazisha dakika ya 36, kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Martin Baturina na kuongeza ushindani wa mechi hiyo ya kuvutia kwa pande hizo zote mbili.

Harry Kane akaendeleza tena makali yake kwa kuiandikia England bao la pili dakika ya 42, akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo wa kikosi hicho, Declan Rice, kisha Croatia ikajibu mapigo dakika ya 45+5, kwa kusawazisha kupitia kwa Petar Musa aliyemazia pasi safi ya Ivan Perisic.

Hadi mapumziko timu hizo zikaenda sare ya mabao 2-2, ingawa, kipindi cha pili England ilirejea kwa kasi na kupata bao la tatu la dakika ya 47, lililofungwa na Jude Bellingham akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa kikosi hicho, Elliott Anderson.

Wakati Croatia ikitafuta kusawazisha, Marcus Rashford aliyetokea benchi akichukua nafasi ya Anthony Gordon akaifungia England bao la nne dakika ya 85 na kuzima matumaini ya kikosi hicho 'Vatreni', kuibuka na ushindi leo.

Mabao mawili aliyofunga Harry Kane yanamfanya kufikisha mabao 10, kwa timu hiyo katika Kombe la Dunia na kufikia rekodi iliyokuwa inashikiliwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho cha 'Three Lions', Gary Lineker aliyefunga pia 10.

Timu hizo zimekutana tena leo katika Kombe la Dunia tangu mara ya mwisho zilipokutana Urusi mwaka 2018, hatua ya nusu fainali na Croatia kushinda mabao 2-1, ya muda wa nyongeza, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Julai 11, 2018.

Hata hivyo, mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa ni katika Michuano ya EURO 2020, iliyochezwa mwaka 2021, kutokana na Maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID-19), ambapo England ilishinda bao 1-0, Juni 13, 2021, lililofungwa na Raheem Sterling.

Timu ya taifa ya England inashiriki kwa mara 17, Kombe la Dunia tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1950, huko Brazil na kuishia hatua ya makundi, japo rekodi bora inayotamba nayo ni ya kuchukua taji hilo mara moja mwaka 1966.

England ilitwaa taji hilo mwaka 1966 kwa kuifunga Ujerumani Magharibi mabao 4–2, katika muda wa nyongeza, ambapo mechi hiyo ilipigwa Julai 30, 1966, chini ya aliyekuwa Kocha, Alf Ramsey wakiongozwa na nahodha wa kikosi hicho, Bobby Moore.

Kwa upande wa Croatia inashiriki mara saba michuano ya Kombe la Dunia tangu ilipoanza kushiriki rasmi kwa mara ya kwanza mwaka 1998 huko Ufaransa na kushangaza mashabiki wengi wa soka duniani, baada ya kikosi hicho kumaliza kikishika nafasi ya tatu.

Katika michuano ya mwaka 1998, aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Davor Suker aliyetamba na timu za Real Madrid na Sevilla za Hispania na Arsenal FC ya England, alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia baada ya kumaliza kwa kufunga mabao sita.

Mafanikio makubwa kwa Croatia ni ya Kombe la Dunia la mwaka 2018, lililofanyika Russia, ambapo ilifika fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yake, japo, ilichapwa na Ufaransa mabao 4-2, Julai 15, 2018 na kumaliza ikiwa nafasi ya pili.

Katika Kombe la Dunia mwaka 2022, Qatar, Croatia ikaendeleza kiwango bora na kuishia nusu fainali baada ya kuchapwa na mabingwa Argentina mabao 3-0, Desemba 3, 2022, japo ilishika mshindi wa tatu kwa kuifunga Morocco mabao 2-1, Desemba 17, 2022.