Ekitike suala la muda Anfield
Muktasari:
- Kuwasili kwa straika huyo Mfaransa, 23, atafanya kikosi cha Liverpool matumizi yake kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kufikia Pauni 270 milioni huku ikiwa bado inamsaka beki wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi ili akawe pacha wa Virgil van Dijk kwenye safu ya ulinzi ya wababe hao mabingwa wa Ligi Kuu England.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA, Hugo Ekitike anatarajia kutambulishwa kuwa staa mpya wa kikosi cha Arne Slot baadaye wiki hii baada ya Liverpool kukubali kulipa Pauni 79 milioni kunasa huduma ya mkali huyo kutoka Eintracht Frankfurt.
Kuwasili kwa straika huyo Mfaransa, 23, atafanya kikosi cha Liverpool matumizi yake kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kufikia Pauni 270 milioni huku ikiwa bado inamsaka beki wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi ili akawe pacha wa Virgil van Dijk kwenye safu ya ulinzi ya wababe hao mabingwa wa Ligi Kuu England.
Ekitike atafanya vipimo vya afya ndani ya saa 48 zijazo na kinachoripotiwa ni kwamba dili la mkataba wa miaka sita limeafikiwa.
Katika kuhakikisha straika huyo anakuwa fiti na kutua zake Anfield kocha wa Eintracht, Dino Toppmoller aliamua kumweka kando kwenye mechi ya kirafiki ya kipigo cha mabao 3-2 ilipomenyana na FSV Frankfurt.
Toppmoller, 44, alisema: “Hakucheza, lakini unaweza kudhani tu ni kitu gani. Ni pigo kubwa, unaweza kuona tulipoteza mchezaji wetu mkubwa kwenye dirisha la majira ya baridi, Omar Marmoush. Mwingine aliyeibuka na kuziba pengo, naye anaweza kuondoka.”
Staa huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain alifunga mabao 22 katika mechi 48 alizocheza msimu uliopita na kuisaidia Frankfurt kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Atatua Anfield kwa ada ya awali ya Pauni 69 milioni pamoja na ziada ya Pauni 10 milioni itakayolipwa baadaye kutokana na viwango vya mchezaji huyo kwenye timu.