Dili la kuwanasa Mbeumo, Eze kuna timu inateseka
Muktasari:
- Arsenal, Manchester United na Tottenham Hotspur zinaingia kwenye vita ya kuwania wachezaji wawili, lakini kwenye orodha hiyo kuna timu moja itaishia kuambulia hasira tu.
LONDON, ENGLAND: MAMBO ni moto. Ndicho unachoweza kusema kwa kile kinachoendelea kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Arsenal, Manchester United na Tottenham Hotspur zinaingia kwenye vita ya kuwania wachezaji wawili, lakini kwenye orodha hiyo kuna timu moja itaishia kuambulia hasira tu.
Spurs inataka kuboresha kikosi chake baada ya ujio wa Kocha Thomas Frank. Imeingia sokoni kuhitaji saini ya fowadi wa Brentford, Bryan Mbeumo ili akaungane na kocha wake huyo wa zamani huko London. Lakini, Mcamerooni huyo, Mbeumo anasakwa pia na Man United.
Spurs imevamia dili hilo la Mbeumo kwa kuongeza Pauni 10 milioni kwenye ofa iliyowekwa mezani na Man United, wao walikuwa tayari kumchukua kwa Pauni 70 milioni.
Vita hiyo inakuja baada ya staa huyo kufunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.
Mbeumo akienda Spurs atakutana na kocha wake wa zamani, Frank. Atapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, shinda ni mchezaji mwenyewe yupo tayari kwenda kujiunga na Man United kwa dili la Pauni 65 milioni na hilo linaweza kukamishwa wiki ijayo.
Kwenye upande huo, Spurs inaona itakwenda kupoteza mbele ya Man United. Imeelekeza mbio kwingineko, ikimtaka staa wa Crystal Palace, Eberechi Eze.
Lakini, kwenye msako wa Eze, Spurs inakabiliwa na vita nyingine ya kupata saini yake na safari hii kutoka kwa mahasimu wao wa London, Arsenal, ambao wanahitaji saini ya Mwingereza huyo kwa nguvu zote, bosi wa usajili wa huko Emirates, Andrea Berta akifanyia kazi hilo.
Kwa maana hiyo, mabingwa hao wa Europa League haionekani itashinda vita yoyote kwenye usajili wa Mbeumo na Eze, ambaye kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachohitaji ilipwe Pauni 68 milioni tu ili ang’oke Selhurst Park.
Kwa maelezo hayo, Spurs ataambulia hasira tu kwenye vita yake na wapinzani wake hao wawili kwenye kusaka saini za wakali hao matata kabisa.