Diaz afunguka kutua Bayern
Muktasari:
- Diaz alisema alichukua uamuzi huo baada ya kumsikiliza Wirtz kwanza, aliyempa mambo mengi ya kuhusu Bundesliga kabla ya kufanya uamuzi wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Allianz Arena.
MUNICH, UJERUMANI: STAA Luis Diaz amesema amezungumza na kiungo ghali wa Liverpool, Florian Wirtz kuhusu Bundesliga kabla ya kukubali dili la kujiunga na Bayern Munich
Diaz alisema alichukua uamuzi huo baada ya kumsikiliza Wirtz kwanza, aliyempa mambo mengi ya kuhusu Bundesliga kabla ya kufanya uamuzi wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Allianz Arena.
Diaz, 28, alijiunga na mabingwa hao wa Ujerumani kwa ada ya Pauni 65.5 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi alipoona ni wakati wa kwenda kukabiliana na changamoto mpya kwingineko.
Baada ya kukubaliana na Liverpool, mabingwa hao wa Ligi Kuu England walikubali kumuuza Diaz kwenda Bayern Munich licha ya kuwapo kwenye timu nyingine kadhaa zilizohitaji huduma yake ikiwamo Barcelona. Licha ya kwamba alihitaji changamoto mpya, Diaz anafichua kwamba kitendo cha kuondoka Anfield kwa ajili ya kwenda kukipiga Munich kilikuwa kama cha kucheza kamali, alipofunga hilo baada ya kufunga bao kwenye ushindi wa 2-1 wa Bayern mbee ya Stuttgart kwenye DFL Supercup wikiendi iliyopita. “Nina furaha na kufarijika kwa namna wikiendi ilivyomalizika,” alisema Diaz.
“Ile ilikuwa mechi yangu ya kwanza ya kimashindano, bao langu la kwanza na taji langu ya kwanza. Nilikuwa na ndoto za kuja hapa kufanikiwa, hivyo nitajitolewa kwa uwezo wangu wote. Nitajaribu kufurahia soka langu.”
Diaz alihamia Bayern baada ya Wirtz kutua Liverpool kwa ada iliyovunja rekodi huko Uingereza. Kiungo huyo wa Kijerumani alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Bayer Leverkusen kilichokuwa chini ya Xabi Alonso msimu uliopita.
“Nilikuwa na uelewa kiasi kuhusu Bundesliga,” alisema Diaz.
“Napenda kutazama soka na michuano yote. Nilipata nafasi ya kuzungumza na Florian na nafahamu nguvu iliyopo kwenye ligi. Natumai nitakuwa na mwanzo mzuri. Nimekuwa kwenye klabu kwa wiki mbili, hivyo nahitaji muda kuzoea.” Diaz na chama lake la Bayern litaanza kampeni mpya ya Bundesliga msimu huu kwa kucheza nyumbani dhidi ya RB Leipzig, Ijumaa.