De Bruyne hana maneno mengi

Muktasari:
- Mbelgiji huyo alitumikia muongo mmoja kwenye klabu hiyo ya Emirates, akibeba mataji sita ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, miongoni mwa mataji yake aliyobeba akiwa na Man City.
NAPLES, ITALIA: KIUNGO Kevin De Bruyne ametoa ujumbe wake wa maneno machache baada ya kukamilisha uhamisho wake wa bure kutoka Manchester City kwenda Napoli.
Mbelgiji huyo alitumikia muongo mmoja kwenye klabu hiyo ya Emirates, akibeba mataji sita ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, miongoni mwa mataji yake aliyobeba akiwa na Man City.
Lakini, Man City iliamua kuachana naye baada ya msimu kufika tamati mwishoni mwa msimu uliopita.
Jambo hilo lilikuwa kinyume na matarajio ya De Bruyne, ambapo kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 alishikwa na butwaa baada ya klabu yake kumruhusu kuondoka.
Kiungo huyo awali alihusishwa na Ligi Kuu Marekani kwenye klabu ya Inter Miami. Lakini, dili la kwenda kujiunga na timu anayochezea Lionel Messi lilikwama baada ya De Bruyne kuchagua kubaki Ulaya.
Na hapo alichagua kujiunga na Napoli, ambayo ilibeba ubingwa wa Serie A msimu uliopita. Napoli, inanolewa na kocha Antonio Conte, ambaye hajawahi kumnoa De Bruyne, lakini hadhi yake ni kubwa kama mmoja wa makocha bora kabisa waliopata kutokea kwenye soka la dunia.
Baada ya dili lake kukamilika Alhamisi iliyopita, ambapo staa huyo alionekana akipiga picha na rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, De Bruyne aliandika ujumbe mfupi, uliosomeka : “Sono qui.” Akiwa na maana ‘Nipo hapa’. Kwenye ujumbe huo, De Bruyne aliambatanisha na emoji ya moyo wa rangi ya bluu.
Na rais wa Napoli, De Laurentiis naye aliposti mtandaoni picha hiyo na kuandika maneno haya: “Benvenuto Kevin!” Akiwa na maana ya ‘Karibu Kevin’ kwa lugha ya Kiswahili.
Napoli imeshinda mataji mawili ya Serie A katika misimu mitatu ya mwisho, huku kwenye kikosi chao kukiwa na wakali wa zamani wa Ligi Kuu England, Romelu Lukaku na Scott McTominay.
Kiungo wa zamani wa Manchester United, McTominay alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu kwenye Serie A msimu uliopita.