Dah! Felix ana jambo zito Milan
Muktasari:
- Felix amekuwa na mwezi wa kwanza mbaya kwenye mkopo wake huko Italia kiasi cha kumfanya apachikwe jina la “majanga” baada ya AC Milan kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bologna.
MILAN, ITALIA: STAA wa Chelsea anayecheza kwa mkopo AC Milan, Joao Felix ameripotiwa mambo yake kwenye vibaya hadi wachezaji wenzake kumtenga ndani ya uwanja.
Felix amekuwa na mwezi wa kwanza mbaya kwenye mkopo wake huko Italia kiasi cha kumfanya apachikwe jina la “majanga” baada ya AC Milan kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bologna.
Mchezaji huyo alicheza dakika 61 katika mechi nyingine ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Torino, Jumamosi kabla ya kutolewa na nafasi yake kuingia Riccardo Sottil.
Gazeti la Italia, Corriere della Sera lilimchambua Mreno huyo na kueleza kuwa mchezaji wa hovyo zaidi aliyekuwa uwanjani baada ya timu yake ya Milan kukumbana na kipigo kwenye mechi ya pili mfululizo.
Felix alijiunga na Milan kwa mkopo kutoka Chelsea kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya baridi. Lakini, kiwango chake kimeshuka tangu alipofunga bao kwenye mechi yake ya kwanza.
Staa huyo aliyewahi kununuliwa kwa Pauni 113 milioni kutoka Benfica kwenda Atletico Madrid, ameshindwa kufunga wala kuasisti kwenye mechi tano mfululizo na zote ameanzishwa. Na kiwango chake kilikuwa hovyo zaidi kwenye mechi ya Bologna na Corriere della Sera likaandika hivi: “Hajaonekana wala kusikika. Hakufanya muvu yoyote, hata wachezaji wenzake walikuwa wanamkwepa.”
Matokeo hayo yameifanya Milan kubaki kwenye nafasi ya saba katika msimamo wa Serie A, pointi nane nyuma ya Top Four. Felix anacheza kwenye timu hiyo kwa mkopo akitokea Chelsea, ambako ana mkataba hadi 2031.