Cristiano Ronaldo arejea mazoezini Al Nassr
Muktasari:
- Nyota huyo alionekana kupitia mitandao ya klabu hiyo akipiga mpira uwanjani, tukio ambalo limeibua hisia njema nchini kwao ambako wanaamini kwamba uwepo wake ungesaidia kuamua matokeo mazuri upande wao katika mechi dhidi ya Mexico.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameonekana akipiga tizi ikiwa ni mazoezi yake ya kwanza tangu alipoondoka katika tiba ya misuli baada ya kuumia na kuibua tabasamu wa nchi yake wakati mechi kati yao na Mexico ikiibua hisia tofauti.
Ingawa ukweli wa kutoonekana kwa Ronaldo katika mechi ya Mexico dhidi ya Ureno bado ni siri ya benchi la ufundi kwani kama ni kupona alishapona kitambo, lakini ukweli ni kwamba ni mchezaji ambaye kila shabiki wa nchi hiyo anataka kumuona wakati wa ufunguzi wa Estadio Azteca, uwanja ambao umeandaliwa kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia 2026.
Hata hivyo, nyota huyo anaendelea na mazoezi, na alionekana akifanya mazoezi saa chache tu kabla ya suluhu kati ya timu hizo mbili za taifa, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu kutoonekana kwake.
Klabu yake ya Al Nassr mara nyingine tena ilitoa picha za Ronaldo akiwa kwenye mazoezi ya siku ya tatu, baada ya kukosa mechi ya kirafiki ya Mexico wakati huu wa kalenda ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Nyota huyo alionekana kupitia mitandao ya klabu hiyo akipiga mpira uwanjani, tukio ambalo limeibua hisia njema nchini kwao ambako wanaamini kwamba uwepo wake ungesaidia kuamua matokeo mazuri upande wao katika mechi dhidi ya Mexico.
Wakati kurudi kwake kumesababisha mjadala fulani, kila kitu kinategemea mchakato wa kupona kutokana na jeraha la misuli lililomzuia kucheza wakati wa mapumziko Fifa. Al Nassr itarudi uwanjani keshokutwa, Ijumaa kukipiga dhidi ya Al Najma katika Ligi Kuu Saudi Arabia, huku matarajio ya kumuona Ronaldo yakiwa bado madogo.